Na SIMON NYALOBI
MWENYEKITI wa Chama Cha Mchezo wa Wavu Mkoa wa Dar es Salaam (DAREVA), Fredy Mshangama, amesema suala la amani lina umuhimu wa kipekee katika kuendeleza michezo.
Akizungumza Dar es Salaam na UHURU, Mshangama alisema kutokana na umuhimu huo, ndiyo maana katika mashindano na vikao vya chama hicho miongoni mwa kauli mbiu wanazozitoa ni kulinda amani.
“Sisi kwetu amani ndiyo kila kitu tukianzisha mashindano lazima twende au tugusie suala la amani kwa sababu tunafahamu mikusanyiko yetu haiwezi kufanyika bila ya kuwepo kwa amani,” alisema.
Mshangama alisema katika kuhakikisha amani inatawala katika chama hicho na mashindano, wamekuwa wakisisitiza umoja miongoni mwao.
Alisema katika ziara za kimichezo alizofanya katika nchi jirani, raia wa nchi hizo wamekuwa wakiwapongeza kuwa Tanzania ni nchi ya amani na ukarimu.
Kuhusu kuanzishwa kwa Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu, Oktoba 29,mwaka jana, kiongozi huyo aliipongeza serikali inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa hatua hiyo.
“Kuwepo Tume hiyo, kunaonyesha ambavyo serikali ipo makini katika
kuendeleza misingi ya amani na utulivu iliyoachwa na waasisi wetu wa Taifa hili,”alisema Mwenyekiti huyo.
Pia, alisema kuongezewa siku 21 kwa tume hiyo kutaongeza ufanisi katika ripoti watakayoikabidhi serikalini.




