Na SUPERIUS ERNEST
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Fasihi aliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Jimbo la Nasarawa cha Nigeria, ni heshima kubwa kwake na Tanzania.
Amesema ameipokea kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, na kwamba inaakisi jitihada zinazofanywa na Watanzania kwa ushirikiano wenye utu katika kulijenga taifa.
Rais Dk. Samia ametunukiwa Shahada hiyo katika Sherehe ya Mahafali ya Nane ya chuo hicho iliyofanyika katika Kampasi Kuu ya Keffi, nchini humo, huku akishiriki kwa njia ya mtandao akiwa Ikulu Chamwino, Dodoma.
Chuo hicho kimemtunuku shahada hiyo Rais Dk. Samia kwa kutambua uongozi wake wa kuwa Kinara wa Nishati Safi ya Kupikia, kuimarisha Afya ya Mama na Mtoto, Taswira nzuri katika masuala ya Uongozi kwa Wanawake Afrika na Kusimamia Masuala ya Biashara hususani kwa Vijana Afrika.
KAULI YA RAIS
Akizungumza baada ya kutunukiwa, Rais Dk. Samia alisema amepokea heshima hiyo kwa unyenyekevu, akieleza mafanikio hayo yanaakisi juhudi za pamoja za Watanzania kuendeleza maendeleo na ushirikiano wa Bara la Afrika.
“Napokea heshima hii kwa unyenyekevu mkubwa. Tuzo hii si yangu pekee, bali inaakisi jitihada za pamoja za wananchi wa Tanzania katika kuendeleza maendeleo, ushirikiano na ustawi wa Bara la Afrika,” alisema Rais Samia.
Aidha, akirejea safari yake ya uongozi, Dk. Samia alisema uzoefu wake hadi kufikia nafasi ya juu ya uongozi wa kitaifa, unatoa chachu ya kuendelea kufungua fursa na kuondoa vikwazo vinavyokwamisha wanawake, vijana kushiriki kikamilifu katika uongozi na uamuzi wa maendeleo barani humo.
SAFARI YA UTUMISHI
Rais alieleza kuwa, safari yake ya utumishi wa umma, ilianzia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), akiwa katika umri mdogo akihudumu kitengo cha utawala, jambo ambalo lilimjengea uzoefu na kumfanya aelewe mahitaji ya wananchi na uwajibikaji.
Aliongeza, aliendelea na uongozi wa serikali katika nafasi mbalimbali hadi alipofikia nafasi ya Makamu wa Rais, mwaka 2015 ambayo alisogea na kupata nafasi ya juu ya kulitumikia taifa na jamii ya kimataifa.
Dk. Samia alisema kiu yake ni kuendelea kuwahamasisha na kuwajengea uwezo wanawake katika katika uongozi, kupata elimu na uwezo wa kujihusisha na shughuli za kiuchumi.
USHIRIKIANO
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Samia aliiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kuanza mazungumzo ya ushirikiano wa kitaaluma na chuo hicho ikiwemo kubadilishana wanafunzi, utafiti na programu za pamoja kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa elimu ya juu na kuchochea maendeleo ya sayansi, utafiti na ubunifu kati ya Tanzania na Nigeria.
HESHIMA
Chuo kikuu hicho kilimtaja Rais Samia kuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya kigeni nje ya Nigeria kutunukiwa Shahada ya Heshima na chuo hicho, na miongoni mwa viongozi wanawake wachache Afrika waliowahi kushika nafasi za juu za uongozi wa kitaifa.
Chuo kikuu hicho cha Jimbo la Nasarawa, Keffi, ni miongoni mwa vyuo vikuu bora nchini Nigeria, kikishika nafasi ya pili kwa vyuo vikuu vya majimbo nchini humo.
Pia, kinashika nafasi ya nane kati ya vyuo vikuu 309 vya nchini humo, na nafasi ya 36 kwa vyuo vikuu vya nchi za Afrika zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Watu wengine mashuhuri waliowahi kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari na chuo hicho ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Amina Mohammed na mfanyabiashara mashuhuri barani Afrika, Aliko Dangote.
TUZO ZINGINE
Aprili mwaka jana, Rais Dk. Samia alitunukiwa Tuzo ya kutambua Wanawake Mashuhuri Afrika (African Iconic Women Recognition Awards), katika sherehe zilizofanyika Lagos, Nigeria.
Pia, Februari mwaka jana, Rais Dk. Samia alipokea Tuzo ya Global Gates Goal-keepers, kutambua uongozi na mchango wake katika kuimarisha afya ya uzazi na kupunguza vifo vya mama na mtoto nchini.
Februari, mwaka huu, Rais Dk. Samia alichaguliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto.
Aidha, Juni 3, mwaka juzi, Chuo kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea (Korea Aerospace University) kilimtunuku Rais Dk. Samia, Udaktari wa Falsafa wa Heshima (Hororis Causa), katika sekta ya anga.
Vilevile, Oktoba 10, mwaka 2023, Chuo Kikuu cha Jawarhalal Nehru, Delhi cha nchini India kimemtunuku PhD ya heshima, Rais Dk. Samia.Shahada hiyo ya Udaktari wa Heshima (Honoris Causa) ametunukiwa kwa mchango wake kwenye diplomasia ya uchumi, maendeleo yanayogusa wananchi moja kwa moja na mchango wake kuimarisha uhusiano wa kimataifa.
Katika michezo Novemba mwaka jana, Rais Dk. Samia, alipokea tuzo kutoka Shirikisho la Kandanda Barani Afrika (CAF) ikiwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya kandanda.




