Na RAMADHANI SEMTAWA
MWAKILISHI Maalumu wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola, Lazarus Chakwera, amewapa nasaha Watanzania kuwa kila mmoja atafute suluhu kutokana na yaliyotokea kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana.
Chakwera ambaye ni Rais mstaafu wa Malawi, alitoa wosia huo kwa Watanzania, jijini Dar es Salaam, alipokutana na Tume ya Uchunguzi wa matukio ya kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka jana.
Akizungumza kwa kifupi baada ya mazungumzo ya kina ya saa mbili na tume hiyo, akiwa katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi nchini, Chakwera alisema: “Kwa kilichotokea Tanzania wakati wa uchaguzi mkuu, kwa sasa kila mtu yupo katika harakati za kutafuta suluhu na kutatua tatizo.”
Chakwera ambaye alionyesha kufurahishwa na kazi za tume hiyo inayoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande, alikutana nayo siku moja baada ya kukutana na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi na vyama vya siasa nchini.
JAJI CHANDE
Akizungumzia waliochojadili na mjumbe huyo maalumu, Jaji mstaafu Chande, alisema “Leo tumempokea Rais mstaafu wa Malawi ambaye ni Mjumbe Maalumu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola. Tulifanya naye mazungumzo ya saa mbili.”
Jaji Chande aliongeza, katika mazungumzo hayo Tume ilimfafanulia utaratibu wa kazi kumwezesha kujua ni nini kinachofanywa kwa mujibu wa hadidu za rejea.
Alifafanua, “Sisi kazi yetu ni kuangalia ushahidi. Hatupelelezi bali tunachunguza ndivyo hadidu zetu za rejea zinavyotueleza. Tumejikita katika ushahidi wa awali.”
Kwa mujibu wa Jaji Chande, Tume ilipangiwa kuonana na Chakwera kumweleza utaratibu huo kama sehemu ya kazi zao za kila siku, kwa mujibu wa hadidu za rejea.
Jaji Chande alisema Tume kama ya nchini inahusika katika mambo makubwa; akitoa mfano ipo hadi Malawi, Kenya, Malaysia na Uganda.
ZIARA YA CHAKWERA
Kwa mujibu wa taarifa ya serikali, Chakwera ambaye atakuwa nchini hadi Aprili 16, tayari ameshakutana na Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmoud Thabit Kombo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge na Wenye Ulemavu, Profesa Palamagamba Kabudi, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Mutungi na vyama vya siasa.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Chakwera anatarajia kukutana na Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, jumuiya zisizo za kiserikali, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jaji George Joseph Kazi na Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo Othman Masoud Othman.
Viongozi wengine anaotarajia kukutana nao ni, Spika wa Bunge Mussa Azzan Zungu, Jaji Mkuu George Masaju, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufaa, Jacobs Mwambegele na Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Asha-Rose Migiro.
Mjumbe huyo pia atakutana na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, na Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete.




