Na AMINA KASHEBA
TIMU ya soka ya Yanga imesema sasa inapeleka nguvu zake katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City.
Yanga itachuana na Mbeya City keshokutwa katika Uwanja wa KMC uliopo Mwenge, Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe alisema Mbeya City ni miongoni mwa timu chache ambazo zimepata pointi mbele ya Yanga.
“Ni muda wa mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi katika uwanja wa KMC kuja kuwauliza Mbeya City kuja kuwauliza waliwezaje kupata pointi kwetu pale Sokoine mkoani Mbeya,” alisema Kamwe.
Ofisa huyo aliwaomba mashabiki wa Yanga kwenda kuisapoti timu yao kwa lengo la kuipa hamasa wachezaji kupata ushindi na kuondoka na pointi tatu muhimu.
“Tuje kwa wingi kusapoti timu yetu haijawahi kutokea tulifanya dhidi ya Tanzania Prisons tukapata ushindi hivyo nawaomba mashabiki wa Yanga kuja kwa wingi katika mchezo huo,” alisema Kamwe.
Katika msimamo wa ligi, Yanga ipo kileleni kwa pointi 44 wakati Mbeya City ipo nafasi ya 12 kwa pointi 17, zote zikishuka dimbani mara 18.




