Na NASRA KITANA
WAKATI Yanga ikihesabu siku na pointi za kutangaza ubingwa, Yanga leo inajitupa tena dimbani kuivaa Dodoma Jiji katika katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pambano hilo, limepangwa kupigwa katika Uwanja wa Airtel uliopo Singida Mjini, kuanzia saa 10:15 jioni.
Yanga itacheza mechi hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Coastal Union ya Tanga na kushinda mabao 3-0.
Kikosi hicho chenye maskani mitaa ya Twiga na Jangwani itaingia dimbani ikiwa kileleni na pointi 54 huku Dodoma Jiji ikishika nafasi ya nane na baada ya kukusanya alama 29 baada ya wote kushuka dimbani 22.
Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Abdihimid Moallin, alisema timu itaingia dimbani huku ikiwa na kumbukumbu ya kufanya vyema katika michezo iliyopita.
“Tunatambua ugumu wa ratiba na mechi yenye upinzani dhidi ya Dodoma Jiji, timu yangu imejipanga kwa ushindi kwa kuwa tunataka alama tatu kwa l engo la kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kutetea ubingwa,” alitamba Moalin.
Moalin amesema pamoja na kikosi chake kutwaa ubingwa mara nne mfululizo, wachezaji wake bado wana njaa ya kubeba ubingwa.
Amesema amezifanyia kazi kasoro zote zilizojitokeza katika mechi iliyopita hivyo anaamini kuwa mechi ya leo haitakuwa na mapungufu.
“Tunataka kuendelea kufanya vizuri na kutopoteza mchezo wowote katika mechi nane zilizobaki na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutetea taji,” aliongeza.
Pia, amesema Mohamed Hussein aliyekuwa majeruhi ameanza mazoezi.
Kipa wa Yanga, Hussein Masalanga, amesema kikosi chao kipo tayari kuendeleza wimbi la ushindi.
“Kwa niaba ya wachezaji wenzangu tumejiandaa vizuri na mchezo wa kesho (leo), kila mmoja wetu anajua umuhimu wake. Kwa sasa lengo letu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo,” amesema Masalanga.
Kocha wa Dodoma Jiji, Amani Josiah, alisema pamoja na Yanga kuwa na kikosi bora, timu yake haitabweteka na kukubali kufungwa.
Alisema timu yake imejipanga kuizuia Yanga au kupata alama zote au walau kugawa pointi.
“Tumefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo wetu na Yanga, tunajua ugumu wa mchezo na tutaingia uwanjani kwa kuwaheshimu wapinzani wetu,” alisema Josiah.
Kocha huyo aliwaomba mashabiki na wapenzi wa timu yao kuendelea kuwapa sapoti ili waweze kufanya vizuri katika michezo iliyobakia ya ligi.




