Na MWANDISHI WETU
MAMLAKA ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imetangaza kupunguza tozo ya Uendelezaji wa Miundombinu Mipya ya Bandari (PID) kutoka asilimia tisa hadi asilimia 4.5 ya kodi ya forodha, hatua inayolenga kuongeza ushindani wa bandari za Tanzania na kutoa nafuu kwa wafanyabiashara pamoja na wadau wa usafirishaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa TPA, Dk George Fasha amesema uamuzi huo umetokana na maoni ya wadau wa sekta ya bandari na dhamira ya Serikali kuhakikisha biashara zinaendelea kwa mazingira rafiki.
Amesema TPA imefanya maboresho hayo baada ya kupokea maoni kutoka kwa wafanyabiashara, waingizaji na wasafirishaji wa mizigo waliotaka kiwango hicho kipitiwe upya pamoja na kuongezewa muda wa utekelezaji wake.
“Tumepunguza ada hii kutoka asilimia tisa hadi asilimia 4.5 kwa kuzingatia hali halisi ya biashara na ushauri wa wadau wetu. Mteja aliyekuwa anatakiwa kulipa shilingi laki mbili sasa atalipa laki moja,” amesema Dk. Fasha.
Kwa mujibu wa TPA, kiwango kipya kitaanza kutumika rasmi Julai Mosi, 2026.
Tozo hiyo ilianzishwa mahsusi kusaidia upatikanaji wa fedha za ujenzi na upanuzi wa miundombinu ya bandari kutokana na ongezeko kubwa la shehena nchini. Awali utekelezaji wake ulianza Machi 8, 2026 baada ya Serikali kuidhinisha marejeo ya ada za bandari za mwambao wa Bahari ya Hindi.
Baadhi ya wadau walieleza kuwa tayari walikuwa wameingia mikataba ya muda mrefu kwa kutumia viwango vya zamani vya ada, huku wengine wakitaka elimu zaidi kuhusu mfumo huo mpya.
TPA imeeleza kuwa mapato yatakayopatikana kupitia tozo hiyo yatatumika kugharimia miradi ya kimkakati ya bandari yenye thamani ya shilingi trilioni 16.1 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa magati mapya katika Bandari ya Dar es Salaam, upanuzi wa Bandari ya Tanga, maendeleo ya Bandari ya Mtwara, ujenzi wa bandari mpya ya Kisiwa Mgao pamoja na maendeleo ya bandari kavu, matenki ya mafuta na miundombinu ya reli na barabara za kusafirisha mizigo.
Kati ya fedha zote zinazohitajika, trilioni 11.2 zinatarajiwa kupatikana kupitia mapato ya huduma za bandari huku sehemu iliyobaki ikitarajiwa kutoka kwenye ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi (PPP).
Dk Fasha alisema uwepo wa chanzo maalum cha fedha kwa ajili ya maendeleo ya bandari utawezesha utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati na kuongeza uwezo wa Tanzania kuhudumia nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Kwa mujibu wa takwimu za TPA, shehena inayopita katika bandari za Tanzania inatarajiwa kuongezeka kutoka tani milioni 32.8 mwaka 2024/25 hadi tani milioni 62 ifikapo mwaka 2030/31.
Katika miezi tisa ya mwaka wa fedha 2025/26 pekee, bandari zote nchini zilihudumia tani milioni 29.6 za shehena pamoja na makasha zaidi ya milioni moja kwa mara ya kwanza katika historia ya sekta hiyo nchini.




