Na JOE NAKAJUMO
SIO siri, kwamba wakazi wengi wa mijini, wanategemea huduma za ‘mama na baba lishe’ kupata milo yote mitatu kuanzia chai asubuhi, chakula cha mchana na usiku.
Mama na baba lishe wanatoa huduma ya chakula maeneo mbalimbali yakiwemo ya shughuli za ujenzi wa miundombinu, ofisini, viwandani, katika gereji na mengine kadhaa.
Kwa Tanzania, watoa huduma hizi za chakula, tangu enzi na enzi walijulikana kama ‘Mama na Baba ntilie,’.
Lakini hivi karibuni Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alikutana nao katika Kongamano la Kitaifa la Baba na Mama Lishe, alikubali pendekezo la kubadili jina kutoka ‘Mama ntilie’ na ‘Baba ntilie’ na kuitwa ‘Mama lishe’ na ‘Baba lishe’.
Akizungumzia pendekezo la kubadili jina wakati wa Kongamano lililofanyika jijini Dar es Salaam Aprili 21, mwaka huu, alisema ‘Mama lishe’ na ‘Baba lishe’ linaendana na hadhi ya kazi wanayofanya.
MAZINGIRA BORA
Alisema serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya kisera na kisheria, kuimarisha sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika uchumi. Aligusia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2050, kwamba sekta binafsi itakuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira.
Dk. Samia alifafanua kuwa, utekelezaji wa maendeleo ya Taifa, utafanyika kwa ushirikiano wa pande tatu. Serikali itachukua sehemu ya utekelezaji kwa asilimia 30, sekta binafsi asilimia kwa asilimia 70 na mashirika ya umma yatakuwa sehemu ya mchakato kwa asilimia nane kwa kushirikiana na serikali na sekta binafsi.
MCHANGO MUHIMU
Mchango wa kundi la ‘Baba na Mama lishe’ ni muhimu na unastahili kuthaminiwa kwa sababu linalisha wananchi na kuwezesha shughuli nyigine za kiuchumi kufanyika kwa ufanisi, Rais alilieleza Kongamano.
Siku chache kabla ya Kongamano, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alieleza umhimu kwa kundi la baba na mama lishe. Sekta hiyo ni moja ya sekta zenye mchango mkubwa katika ajira na uchumi, hivyo haiwezi kuachwa nyuma katika jitihada za maendeleo ya Taifa.
Kuelekea mwaka 2050, serikali inalenga kuona sekta binafsi inachangia kiasi kikubwa katika uchumi, baba na mama lishe wakiwa sehemu muhimu ya mnyororo huo kuyafikia malengo yanayokusudiwa.
DIRA 2050
Shabaha ya Dira 2050, ambayo utekelezaji wake unaanza Julai Mosi mwaka huu, ni kuchochea ukuaji wa Pato la Taifa kutoka dola za Marekani sh. bilioni 88.4 za sasa hadi sh. dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Wastani wa pato la mtu mmoja lilifikia thamani ya dola za Marekani 7,000 kwa mwaka.
Baadhi ya malengo mengine ni kuiweka Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 10 bora Afrika katika uzalishaji chakula. Mtanzania kuishi wastani wa miaka 75 yenye afya na furaha kutoka miaka 68 ya sasa.
Kutokana na umuhimu wa baba na mama lishe kwa jamii na katika ujenzi wa uchumi, serikali imeamua kuweka mfumo rasmi wa kuwatambua na kuwaongoza kuhakikisha wanatoa huduma katika mazingira salama na yenye viwango vinavyokubalika.
Lengo la Kongamano la Kitaifa la Baba na Mama Lishe, lilikuwa ni kuwakutanisha kutoka mikoa yote 31 ya Tanzania, ikiwemo mitano ya Zanzibar. Madhumuni ya kuwakutanisha ni kuwasikiliza na kuwatambua rasmi na kuweka msingi wa namna bora ya kuwawezesha.
Kila mkoa uliwakilishwa na mama lishe wanne viongozi, wakisindikizwa na maofisa wa maendeleo ya jamii mmoja kila mkoa.
SABABU URASIMISHAJI
Serikali imeweka wazi urasimishaji wa kundi la baba na mama lishe hautalenga kuwaongezea mzigo wa kodi, bali ni hatua ya kuwawekea mazingira rafiki ya kufanya kazi kwa usalama na ufanisi zaidi.
Hatua ya kwanza ni kuwasajili kidijitali baba na mama lishe wote nchini, kujua idadi yao, maeneo wanayofanyia kazi na changamoto wanazokutaka nazo.
Kila mmoja atakuwa na utambulisho utakaounganishwa na taarifa zake na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA). Hii itasaidia kuwafikia kwa urahisi na kuwapatia huduma mbalimbali za maendeleo.
Jambo jingine muhimu katika usajili wao, ni kuunganishwa na fursa za mikopo nafuu, ikiwemo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri na mikopo kutoka taasisi za fedha na kidogo inayotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi maalumu.
Kwa muda mrefu mama na baba lishe, wamekuwa wakifanya kazi bila mwongozo maalumu, hali inayochangia kuwapo kwa hatari za kiafya kwa watumiaji huduma.
MAAGIZO WIZARA TANO
Rais Dk. Samia katika hotuba yake kupitia Kongamano, alitoa maagizo kwa wizara tano kuhakikisha kundi la baba na mama lishe linapata manufaa kiuchumi.
Ameitaka Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), kutenga na kuendeleza maeneo rasmi ya kufanya biashara kwa mama na baba lishe wafanye kazi katika mazingira bora na heshima.
Wizara ya Nishati, imeagizwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kupunguza gharama za uendeshaji, kulinda mazingira na kuboresha afya za wahudumu.
Elimu ya afya ni jambo la msingi, hivyo Wizara ya Afya inatakiwa kuimarisha utoaji elimu ya lishe na usalama wa chakula, ulinda afya za walaji na kuboresha viwango vya huduma.
Kwa upande wa Wizaza ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wanawake na Makundi Maalumu, inatakiwa kushirikiana na taasisi zingine kutoa mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa mitaji kwa baba na mama lishe.
Wizara ya Fedha nayo inahusika katika kusaidia sekta hii na Rais imeitaka kuweka mazigira rafiki ya kisera na kisheria kuwawezesha wafanyabiashara wadogo kunufaika na huduma za kifedha.
DK.MWIGULU AMUOKOA MAMA LISHE
Ushahidi kwamba mama na baba lishe ni muhimu katika kutoa huduma zao kwa jamii, ulidhihirika wakati wa ziara ya Waziri Mkuu,Dk. Mwigulu Nchemba, mkoani Manyara, Februari mwaka huu.
Waziri Mkuu Dk. Mwigulu,aliliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, kumtafuta mkandarasi Bakema Said Bakema aliyejenga madarasa kataika Shule ya Msingi Dosidosi, wilayani Kiteto, kuhakikisha anamlipa mama lishe Mariamu Mwinyikai sh.1,002,000 na riba.
Mama lishe huyo alimlalamikia Waziri Mkuu katika mkutano wa hadhara, kwamba hakulipwa fedha ya kuwalisha wafanyakazi wa mkandarasi kwa miaka sita hadi wakati huo wa ziara.
Waziri Mkuu alinukuliwa akisema “Mkuu wa wilaya huyu mkandarasi yuko wapi, hivi huyu mama mnachukua milioni moja yake kwa miaka sita, sasa mkuu wa wilaya mtafuteni po pote alipo alipe na riba ya fedha alipe mara mbili ya hiyo fedha aliyochukua.
“Mtume kamanda wa polisi, amsake po pote alipo,haya mambo ya kuoneaonea wanyonge haya,mama kaonane na katibu wangu akupe nauli ya kurudia,”
Haikubaliki kwa mama huyo kutoa huduma ya chakula kwa mafundi wa mkandarasi huyo halafu asilipwe fedha zake kwa kipindi cha muda mrefu, alisema Waziri Mkuu kwa mshangao.
MBUNGE AJITOSA
Katika kuwasaidia mama lishe, Mbunge wa Viti Maalum (Vijana) Zainab Abdallah, alisema atahakikisha anawaunganisha mama lishe katika mifumo rasmi ya kiuchumi. Alisema kundi hilo lina msaada mkubwa kwa jamii.
Mbunge alisema atahakikisha watalamu kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma(PPRA) wanatoa mafunzo na kuwaunganisha wanawake katika mfumo.
Naye Meneja wa Uhusiano wa Kimkakati wa Airtel, Jemima Masimba alisema mkakati ni kuimarisha ujumuishi wa kifedha na uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake hususan mama lishe.
SHUKRANI KWA MIKOPO
Mwenyekiti wa mama na baba lishe Mkoa wa Dodoma Ester Mwansasu, alisema kundi hilo linaendelea kumuunga mkono Rais Dk. Samia kwa sababu amewawezesha kupata mikopo iliyowanyanyua kibiashara.
Anasema mikopo waliyopewa haina riba,ila wanaomba masharti yapunguzwe watu wengi wanufaike.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wanawake na Makundi Maalum, Maryprisca Mahundi, aliliambia Bunge linaloendelea na mkutano wake Dodoma, kwamba serikali ipo hatua za mwisho kuanza utoaji mikopo maalumu kwa wanawake kupitia mradi wa pamoja unaotekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia, ikiwa na lengo kuongeza wigo wa wanufaika.
UTATUZI WA CHANGAMOTO
Katika hatua nyingine serikali imetangaza hatua za utatuzi wa changamoto za mfumo wa mtandao katika maombi ya mikopo ya asilimia 10, kwa wanawake wanaoishi maeneo ya vijijini.
Akijibu swali Bungeni, Naibu Waziri TAMISEMI, Festo Ndugange, alisema katika kutatua changamaoto za mfumo mtandaoni, katika maombi ya asilimia 10 kwa makundi maalumu yakiwemo ya wanawake wa vijijini, serikali itawawezesha waombaji kufanya usajili wa maombi ana kwa ana, ambapo maofisa maendeleo ya jamii kupitia kamati za kata za huduma za mikopo huvisaidia vikundi visivyokuwa na uwezo wa kutumia mfumo wa kieletroniki wa WEZESHA.
(Mawasiliano na Mwandishi WhatsApp 0784291434;email nakajumoj@gmail.com)




