• ePaper
Saturday, May 30, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Makala

JITIHADA ZA KUTOKOMEZA FISTULA TUMAINI JIPYA KWA WANAWAKE

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
May 27, 2026
in Makala
0
JITIHADA ZA KUTOKOMEZA FISTULA TUMAINI JIPYA KWA WANAWAKE
0
SHARES
3
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

Na BALTAZAR MASHAKA

WAKATI dunia ikiendelea kuadhimisha juhudi za kuboresha afya ya mama na mtoto, Tanzania nayo inaongeza kasi ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa fistula kwa lengo la kuutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030.

Serikali, kupitia Wizara ya Afya kushirikiana na wadau mbalimbali wa afya, imeendelea kusisitiza umuhimu wa kupeleka huduma na elimu hadi ngazi ya jamii kuwafikia wanawake walio katika hatari ya kupata ugonjwa huo.

Kwa miaka mingi, wanawake wengi wanabeba maumivu makubwa kimya kimya kutokana na ugonjwa wa fistula tatizo linaloathiri afya, heshima na maisha yao ya kila siku.

Wengi wao, wamejikuta wakitengwa na jamii, kuvunjika moyo na hata kupoteza matumaini ya maisha kwa sababu ya hali hiyo.

Hata hivyo, juhudi za serikali na wadau wa sekta ya afya zinaendelea kuleta nuru mpya kwa wanawake hao kupitia huduma za matibabu, elimu na kampeni za kuutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.

Licha ya juhudi kubwa zinazofanywa na serikali kuboresha huduma za afya ya uzazi, bado baadhi ya wanawake wanaendelea kupata fistula kutokana na changamoto mbalimbali za kijamii na kiuchumi na ucheleweshaji wa kupata huduma za afya wakati wa ujauzito na kujifungua.

Rai ya kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya fistula ilitolewa Mei 21, mwaka huu, mkoani Tabora na Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Boniface Marwa, katika kongamano lililofanyika Hospitali ya Rufaa Maalumu ya Nkinga kuelekea maadhimisho ya siku ya kimataifa ya kutokomeza Fistula Duniani yaliyofanyika mkoani humo.

Kwa mujibu wa Dk. Marwa, changamoto za kijamii, umasikini, umbali wa vituo vya afya na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, ni miongoni mwa sababu zinazochangia wanawake wengi kuendelea kupata tatizo hilo.

“Fistula ni moja ya matatizo makubwa ya kiafya yanayowaathiri wanawake wengi hasa maeneo yenye changamoto za huduma za afya. Mara nyingi ugonjwa huo, husababishwa na uchungu wa muda mrefu wakati wa kujifungua bila kupata huduma sahihi kwa wakati, na kusababisha majeraha katika njia ya uzazi, hivyo mwanamke kushindwa kudhibiti mkojo au haja kubwa,” alisema.

Mganga Mkuu huyo wa Mkoa wa Tabora, alisema mbali na madhara ya kiafya, fistula huathiri maisha ya kijamii na kiuchumi ya wanawake wengi, baadhi yao hukumbwa na unyanyapaa, kutengwa na hata kupoteza matumaini ya maisha kutokana na hali hiyo.

“Fistula siyo tu tatizo la kiafya, ni changamoto ya kijamii inayomnyima mwanamke haki ya kuishi kwa heshima. Tunapaswa kuongeza elimu kwa jamii na kuhakikisha wajawazito wanapata huduma mapema,” alisema.

Dk. Marwa alisema, uwepo wa visa vya fistula unaonesha umuhimu wa kuongeza elimu kwa jamii kuhusu afya ya uzazi, umuhimu wa wajawazito kuhudhuria kliniki mapema na kujifungulia vituo vya afya vyenye wataalamu na vifaa vya kutosha.

Alisisitiza kuwa, wataalamu wa afya ngazi ya jamii wanatakiwa kupewa nafasi kubwa zaidi ya kutoa elimu kuhusu fistula kusaidia kubadili mtazamo wa jamii na kuongeza uelewa kuhusu namna ya kuzuia ugonjwa huo.

Maisha ya Maumivu na Unyanyapaa kwa wanawake wengi waliowahi kuugua fistula, maisha yao yalibadilika ghafla baada ya kupata tatizo hilo.

Mmoja wa wanawake waliowahi kuathirika na fistula na baadaye kupata matibabu Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Maretha James, alisema alipata tatizo hilo baada ya kupata uchungu wa muda mrefu wakati wa kujifungua mtoto wake wa kwanza.

Alisema, baada ya kujifungua alianza kushindwa kudhibiti mkojo hali iliyomfanya kuishi maisha ya fedheha na kujitenga na jamii.

“Nilikuwa nikilia kila siku. Watu walinicheka kutokana na harufu ya mkojo. Hata baadhi ya ndugu waliniona mzigo. Nilipoteza furaha ya maisha na sikuamini kama ningepona,” alisema mwanamke huyo kwa masikitiko.

Alisema baada ya kupata taarifa kuhusu huduma za matibabu ya fistula katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, alifanyiwa  upasuaji na sasa amepona kabisa na kurejea, kuendelea na shughuli zake za kawaida.

“Leo ninaishi maisha ya kawaida tena. Nawaomba wanawake wasiogope kutafuta matibabu mapema kwa sababu fistula inatibika,” alisema.

Chanzo na Namna ya Kujikinga

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, fistula hutokea zaidi pale mwanamke anapopata uchungu wa muda mrefu bila msaada wa kitaalamu wakati wa kujifungua, hali inayosababisha majeraha katika njia ya uzazi.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Igalla, wilayan Ukerewe, Dk. Tumai Baumba, alisema wanawake wengi wanaofika hospitalini hupata fistula kwa sababu ya kuchelewa kufikishwa katika vituo vya afya au kujifungulia nyumbani bila usaidizi wa wataalamu.

“Mbali na kuchelewa kufika hospitalini, uchungu pingamizi ni moja ya visababishi vya fistula, hii inatokana na nyonga ndogo za mama kuliko ukubwa wa mtoto, au mtoto kuwa na kichwa kikubwa,” alisema.

Aliongeza kuwa, uchungu pingamizi unaweza kusababisha mama kuchanika mfuko wa kizazi wakati wa kujifungua, saratani ya kizazi ama via vya uzazi, inameng’enya kibofu cha mkojo na eneo la haja kubwa.

“Kuna aina mbili za fistula, inayohusisha mawasiliano kati ya kibofu cha mkojo na uke, kuna kuwa na tundu ambapo mkojo hutoka mfululizo bila kizuizi. Ya pili ni ya utumbo wa haja kubwa unaowasiliana na uke, hii huwapata hasa kinamama wanaochanika njia ya uzazi, endapo mama hatatibiwa vizuri anaweza kupata fistula,”alisema.

Mtaalamu huyo wa afya alisema, tatizo hilo linaweza kuzuilika kwa wajawazito kuhudhuria kliniki mara kwa mara, kujifungulia hospitalini na kupata huduma za dharura kwa wakati.

“Wanawake wengi wanaopata fistula wanatoka maeneo ya vijijini ambako huduma za afya bado ni changamoto. Elimu kwa jamii ni muhimu kuondoa imani potofu na ucheleweshaji wa kutafuta huduma,” alisema.

 JUHUDI ZA SERIKALI

Kwa upande wake, Mratibu wa Huduma za Fistula kutoka Wizara ya Afya, Fidea Obimbo, alisema serikali inaendelea kuimarisha afua mbalimbali za kupambana na fistula kushirikiana na wadau wa sekta ya afya ikiwemo chama cha wanaotoa huduma hizo nchini.

Alisema mikakati inayotekelezwa inalenga kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto, kuongeza upatikanaji wa huduma za upasuaji na elimu kwa jamii kuhusu afya ya uzazi.

“Tunataka kuhakikisha hakuna mwanamke anayeteseka kwa ugonjwa unaozuilika na kutibika. Ndiyo maana tunaendelea kuimarisha huduma hadi ngazi ya jamii. Pia, mikakati inayotekelezwa inalenga kufanikisha malengo ya kitaifa na kimataifa ya kutokomeza fistula kupitia sera ya afya inayosisitiza uboreshaji wa huduma za afya ya mama na mtoto.” alisema.

Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Fistula Duniani mwaka huu inasema, ‘Afya ni haki ya msingi ya kila mwanamke, wekeza kutokomeza fistula na majeraha yatokanayo na uzazi’.

Afya ya uzazi na kuhakikisha wanawake wote wanapata huduma bora bila ubaguzi au vikwazo vya kijamii na kiuchumi, imeendelea kuhamasisha jamii kutambua kuwa, afya bora ya mama ni msingi wa maendeleo ya taifa.

Wataalamu wa afya wanaamini kuwa, lengo la kutokomeza fistula ifikapo mwaka 2030, linawezekana iwapo kutakuwa na uwekezaji mkubwa katika huduma za afya ya uzazi, elimu kwa jamii na upatikanaji wa huduma za upasuaji kwa wanawake walioathirika.

Mapambano dhidi ya fistula siyo jukumu la sekta ya afya pekee, ni wajibu wa jamii nzima kuhakikisha hakuna mwanamke anayepoteza heshima, matumaini na furaha ya maisha kutokana na tatizo linaloweza kuzuilika na kutibika.

Kadri juhudi zinavyoendelea kuimarishwa, matumaini yanaongezeka kuwa Tanzania inaweza kufikia lengo la kutokomeza fistula ifikapo mwaka 2030 na kurejesha tabasamu kwa maelfu ya wanawake waliokuwa wakiishi katika maumivu na unyanyapaa.

Previous Post

KAMPENI ZA KUMNADI EMMANUELA ZINAVYOPAMBA MOTO ISMANI

Next Post

RAIS DK. SAMIA AWAFUNDA MAJAJI ALIOWAAPISHA

Next Post
RAIS DK. SAMIA AWAFUNDA MAJAJI ALIOWAAPISHA

RAIS DK. SAMIA AWAFUNDA MAJAJI ALIOWAAPISHA

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

KATIBU MKUU CCM ZIARANI UCHINA

KATIBU MKUU CCM ZIARANI UCHINA

2 months ago
WACHEZAJI WA TEMBO WARRIORS

TEMBO WARRIORS KUFANYIWA MCHUJO

9 months ago

Popular News

  • RAS: UTUNZAJI MAZINGIRA AJENDA YA KIPAUMBELE KWA MKOA WA MWANZA

    RAS: UTUNZAJI MAZINGIRA AJENDA YA KIPAUMBELE KWA MKOA WA MWANZA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • UPELE UMEPATA MKUNAJI STARS

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • ‎ RAIS DK. SAMIA: POLISI MSIDHARAU TAARIFA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • DK. MWIGULU ATETA NA WAZIRI MKUU WA CONGO BRAZZAVILLE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • MASTAA YANGA WAUTAJA UBINGWA LIGI KUU BARA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?