Na MWANDISHI MAALUMU, Morogoro
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme -WFP), limesema litaendeleza ushirikiano na serikali ya Tanzania katika kuhakikisha masuala ya menejimenti ya maafa yanaendelea kutekelezwa kwa tija na malengo yaliyokusudiwa kwa kuimarisha uwezo wa kitaalamu na Kiteknolojia kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Hayo yameelezwa na Naibu Mkurugenzi wa WFP Tanzania, Christine Mendes wakati wa ufunguzi wa warsha ya zoezi la uigaji la uratibu wa utoaji wa misaada ya kibinadamu na usafirishaji wakati wa dharura inayoendelea mkoani Morogoro.
Christine amesema ushirikiano hususan katika kuwezesha utekelezaji wa Mradi wa Field-Based Preparedness Project (FBPP), ambapo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, mradi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uwezo wa taifa katika sekta ya utoaji wa misaada ya kibinadamu na usafirishaji.
Aidha, alieleza zoezi la uigaji la uratibu wa utoaji wa misaada ya kibinadamu na usafirishaji wakati wa dharura linawakilisha hatua muhimu katika kuendelea kujitolea kwa Tanzania katika kuimarisha utayari wa kitaifa katika uratibu wa masuala ya maafa.
“Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Mradi wa Matayarisho ya Uwandani (FBPP) umetoa mafanikio yaliyounganishwa ambayo yameimarisha kwa kiasi kikubwa utayarishaji wa vifaa na mfumo wa kukabiliana na dharura wa Tanzania,” alisema.
Ameongeza WFP itaendeleza ushirikiano wake na serikali na kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono masuala ya menejimenti ya maafa kuyafikia matarajio kwa pamoja kwa kuwa na mfumo wa kukabiliana na hali ya dharura wa kitaifa wenye kasi zaidi, ulioratibiwa vyema na unaostahimili zaidi wenye uwezo wa kutoa hatua za kibinadamu kwa wakati unaofaa.
“Tutumie fursa hii kikamilifu, siyo tu kupima mifumo, lakini kuimarisha mifumo, hivyo tuthibitishe tena dhamira yetu ya pamoja ya kujitayarisha kwa kuwajibikana kulenga kwa dhati kuokona maisha,” amesisitiza Christine.







