Zanzibar
Na HANIFA RAMADHANI
ZANZIBAR ni neema tu! Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kuzindua mabasi yanayotumia umeme hatua inayolenga kupunguza uchafunzi wa mazingira na kuimarisha matumizi ya nishati safi.
Dk. Mwinyi amesema uzinduzi huo ni mkakati wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuiwezesha Zanzibar kuwa kinara kwa matumizi ya usafiri wa magari yanayotumia umeme.
Akizindua huduma za usafiri huo wa umma na kituo cha mabasi hayo, Dk. Mwinyi alisema utekelezaji wa mpango huo ni sehemu ya mkakati wa serikali kuhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira, kupunguza utegemezi wa mafuta na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema matumizi ya vyombo vinavyotumia umeme yataongeza ufanisi wa sekta ya usafiri na kuiwezesha Zanzibar kuwa mfano bora wa matumizi ya nishati mbadala Afrika Mashariki.
Alibainisha kuwa, hatua hiyo ni mwendelezo wa mkakati wa serikali kubadilisha vyombo vya usafiri wa umma kutoka kutumia mafuta kwenda umeme, hivyo alihimiza sekta binafsi kuinga mfano huo.
“Leo (jana) nimefurahi kupata fursa ya kuweka historia ya kuanzisha vyombo vya usafiri wa umma vinavyotumia umeme na muda mfupi ujao, tutaendeleza hatua hizi ili njia zote nchi nzima ziwe na vyombo vinavyofanana na hivi tunavyovizindua,” alisema.
Aidha, alisema ufunguzi wa kituo hicho ni mwendelezo wa jitihada za serikali kuimarisha haiba ya mji wa Zanzibar na kutoa huduma bora za usafiri kwa wananchi.
Dk. Mwinyi alibainisha kuwa, mradi huo ni mwanzo wa mambo makubwa yanayotarajiwa kumiminika visiwani humo na kuahidi kuendelea kuboresha usafiri wa umma unaotumia umeme.
“Tuliadihi teksi za baharini, treni zinakuja, hivyo wale ambao wana fitina, husda kwa kauli tunazozitoa nawaambia kwamba tumeshajipanga katika utekelezaji na ndiyo maana tunatembea kifua mbele.
“Mabasi yanaonekana, vituo vinaendelea kujengwa na tutaendelea kutekeleza ahadi zetu tulizozitoa ili Zanzibar ibadilike katika nyanja zote,” alisema.
Aliutaka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kuhakikisha vituo vinavyoendelea kujengwa vikamilike kwa wakati wananchi na wageni wanufaike na huduma hiyo.
Alitumia nafasi hiyo kuwapongeza wahusika wa mradi huo kuweka viwango maalumu vya nauli hususan kwa wazee wastaafu na wanafunzi.
Rais Mwinyi aliwasihi wananchi kuendelea kuiunga mkono serikali na kuwa walinzi wa miundombinu iendelee kuleta maendeleo hususan katika sekta ya usafiri.
ZANZIBAR KUBADILIKA KIUCHUMI
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Juma Malik Akil, alisema mradi huo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane inayongozwa na Dk. Mwinyi kuibadilisha Zanzibar kiuchumi.




