Na NASRA KITANA
BAADA ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Geita Gold kocha wa Yanga, Manqoba Mngqithi amejifunza kuwa kadi nyekundu aliyoonyeshwa kiungo wa timu hiyo, Stephane Aziz KI imewapa uzoefu wa kucheza muda mrefu wakiwa pungufu.
Pia, alisema tukio hilo, limeisaidia timu kujenga tabia ya kujiandaa kwa changamoto zinazoweza kutokea katika msimu mzima.
Yanga juzi iliitandika bao 1-0 timu ya Geita Gold katika mchezo uliopigwa Uwanja wa KMC Dar es Salaam.
Bao la ushindi lilipachikwa wavuni na beki wa timu hiyo, Farouk Koumara katika dakika ya 54 ya mchezo.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Mngqithi alisema hakuridhishwa na uamuzi wa mwamuzi kumpa kadi nyekundu Aziz KI kwa vile hakuona nia ya kumdhuru mpinzani.
Hata hivyo, kocha huyo alifurahishwa na namna wachezaji wake walivyopambana licha ya kumkosa Aziz Ki.
Alisema changamoto kubwa ilikuwa kupoteza uwezo wa kufanya presha ya juu kusaka mabao zaidi.
Hata hivyo, kocha huyo alisema waliamua kubadilisha baadhi ya mipango yao kipindi cha pili na wachezaji wake kufanikiwa kupambana kupata matokeo mazuri.
Mngqithi aliwashukuru wachezaji wake kwa kuipambania timu mwanzo mwisho kuhakikisha wanafanya vizuri na kufikia malengo waliojiwekea.
“Ukweli kadi nyekundu alionyeshwa Aziz Ki imewaongezea wachezaji wangu ubora na uzoefu wa kucheza muda mrefu wakiwa pungufu,” alisema Mngqithi.
Kocha huyo alifafanua kuwa malengo yao ni kuhakikisha wanapata alama tatu katika kila mchezo.
Mngqithi amefurahishwa na kiwango kilichoonyeshwa na mshambuliaji wa timu hiyo, Clement Mzize kuwa kizuri na ana imani, atafanya vizuri licha ya kukaa nje kwa takribani miezi saba bada ya kupata majeraha.
Kocha huyo alisema Mzize ni miongoni mwa wachezaji muhimu katika mipango yake na anatamani aendelee kuwa fiti msimu huu ili aisaidie timu kushinda mabao mengi zaidi.
Aidha, Mngqithi alisema anasubiri kwa hamu kurejea kwa beki Dickson Job, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na kikosi kamili na wachezaji wote wakiwa katika afya njema.
Mngqithi alisema kuwa kuhusu baadhi ya wachezaji aliowapumzisha katika mchezo wa dhidi ya Geita Gold, hawakuwa na majeraha, bali aliamua kuwapa mapumziko kutokana na kucheza michezo kadhaa mfululizo.
Kocha wa Geita Gold, Zuberi Katwila, alisema kadi nyekundu aliyoonyeshwa Aziz KI dakika ya 18, haikufanya timu hiyo kuwa dhaifu.
“Kiukweli pamoja na mchezaji wa Yanga kupewa kadi nyekundu, timu yao haikuwa dhaifu na wao kushindwa kutumia vyema nafasi waliokuwa nayo ya kupata ushindi, hivyo wanaenda kurekebisha kasoro zilizojitokeza,” alisemaila.
Katwila alisema ana imani kubwa na wachezaji wake kwani wamefanya makosa na wapinzani wake wameyatumia vyema kupata ushindi.




