Na AMINA KASHEBA
KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema anaamini kikosi chake kitafanya vyema katika msimu ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya Shirikisho la Afrika (CAFCC).
Akizungumzia maandalizi ya msimu mpya kocha huyo amesema hivi sasa kikosi chake kipo vizuri japokuwa bado anaendelea kufanya uboreshaji wa baadhi mambo madogo madogo kuhakikisha wachezaji wote wanakuwa fiti kupambana katika michuano mbalimbali msimu mpya.
Amesema wanasubiri wachezaji wengine waungane na wanzao kuendelea na programu mbalimbali za mazoezi kuelekea katika ligi na michuano ya CAFCC.
“Tulianza na mazoezi ya utimamu wa mwiliu baada ya mapumziko ya muda mrefu, hivi sasa tumeshaingia uwanja wa mazoezi kuendelea kujifua.
“Kikosi changu kipo vizuri japokuwa kuna vitu vya kufanyia uboreshaji, tunaamini tutafanya vyema msimu mpya utakapoanza na kufikia malengo.
“Tuna muda wa kutosha kujiandaa tunajiamini tunakwenda vizuri, tunapaswa kuyafanyia kazi baadhi ya maeneo kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Ibenge.
Kocha huyo amesema hivi sasa yupo katika kuyafanyia kazi madhaifu ya kikosi chake kipindi hiki cha maandalizi.
“Maandalizi yanakwenda vizuri pia wachezaji wangu wanaonyesha kujituma mazoezini kitu ambacho kinaniongezea imani kwamba tutakuwa na msimu bora zaidi,” amesema.