Na MWANDISHI WETU
BODI ya Wakurugenzi ya klabu ya Simba, imefikia makubaliano Meneja Mkuu, Dimitar Pantev kusitisha mkataba wa kuinoa timu hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na bodi hiyo imeeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa na pande zote mbili jana.
Pantev pamoja na wasaidizi wake wawili wamesitishiwa miakataba yao na hivi sasa kikosi hicho kitakuwa chini ya kocha Seleman Matola.
Hata hivyo, taarifa ya bodi hiyo imeeleza kuwa, mchakato wa kupata kocha mpya unaendelea kufanyika hivi sasa.
Pantev ni raia wa Bulgaria, ana umri wa miaka 49 alijiunga na Simba kama Kocha Mkuu akichukua nafasi ya Fadlu David aliyeachana na Klabu hio mapema mwezi Oktoba, mwaka huu.
Kama meneja Dimitar Pantev amewahi kuzifundisha timu za Vladislav Varna, Shabla, klabu ya futsal Grand Pro Varna, timu ya Taifa ya futsal ya Bulgaria.
Amewahi kuzinoa timu za Spartak Varna, klabu ya Palestina Alshoban Almuslimin Hebron, Svetkavitsa Targovishte, Victoria United ya nchini Cameroon.
Timu nyingine ni klabu ya Sierra Leone ya Johansen na Orapa United ya nchini Botswana.
Pantev alianza kazi yake ya usimamizi kama mkufunzi wa vijana katika Jiji la Varna. Wakati wa msimu wa 2008-09 alikuwa mkufunzi msaidizi wa Dobrudzha Dobrich.
Pia alifanya kazi kama kocha Mkuu wa Vladislav Varna na Shabla katika Ligi ya Bulgaria.
Amewahi kushinda mataji matano mfululizo ya Ligi Kuu ya Bulgarian Premiere Futsal, akiiongoza klabu hiyo,pia alisimamia timu ya taifa ya Bulgaria ya futsal mara mbili.
Mnamo Julai 2022, Pantev aliteuliwa kuwa meneja wa Victoria United huko Cameroon.
Mwezi Machi 21, mwaka 2024, Pantev alirudi Victoria United, baadaye aliongoza Victoria kwa kutwaa taji lao la kwanza la Elite One katika historia ya klabu hiyo.
Januari 23, mwaka huu, Pantev aliteuliwa kama meneja wa Gaborone United, akiongoza timu hiyo kutwaa taji la Ligi Kuu ya Botswana katika msimu wake wa kwanza katika klabu hiyo.




