Na ABDUL DUNIA
KAIMU Kocha Mkuu wa Simba, Selemani Matola, leo atakabiliwa na mtihani wake wa kwanza atakapoiongoza timu hiyo katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City.
Mtihani huo kwa Matola, unakuja kutokana na rekodi nzuri iliyo nayo Wekundu hao wa Msimbazi waliovuna pointi tisa katika mechi tatu walizocheza, ndiyo timu pekee ambayo haijapata matokeo tofauti na ushindi.
Katika mechi tatu zilizopita, Simba imeshinda dhidi ya Fountain Gate (3-0), Namungo (3-0) na JKT Tanzania (2-1) ambapo Matola anatakiwa kuendeleza moto huo wa ushindi katika ligi hiyo.
Wapinzani wa Simba, Mbeya City wenyewe hadi leo, wamefanikiwa kuvuna pointi nane katika mechi tisa ilizocheza katika ligi hiyo yenye ushindani mkubwa.
Mbeya City ilikubali vichapo dhidi ya Mashujaa (1-0), Coastal Union (2-0) na kufungwa 1-0 na timu ya Namungo .
Pambano la Simba na Mbeya City lim epangwa kuanza kufanyika saa 1:00 usiku katika mechi itakayopigwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.
Matola ambaye ataliongoza benchi la ufundi la Simba kwa mara ya kwanza ikiwa ni siku kadhaa tangu alipokaimu mikoba hiyo baada ya klabu hiyo kuachana na aliyekuwa Meneja Mkuu, Dimitar Pantev.
Katika mtanange wa leo, Simba itapaswa kuvuna pointi tatu ili kuendeleza rekodi yake ya ushindi kwa asilimia 100 katika ligi hiyo wakati Mbeya City ikihitaji kupata ushindi wake wa kwanza baada ya kupoteza mechi tatu mfululizo msimu huu.
Akizungumza Dar es Salaam, Matola alisema amekiandaa vyema kikosi chake kuhakikisha kinavuna pointi tatu katika mtanange huo.
“Tumejielekeza zaidi katika ligi, tutahakikisha tunafanya vyema. Ligi ni ngumu na tunaichukulia kwa umuhimu sana mechi ya kesho (leo) na tumejiandaa vizuri kupata ushindi.
Tutatengeneza timu kwa uwiano sasa katika kushambulia na kuzuia, tutaangalia ubora wetu upo wapi kujua tunapataje ushindi,” alisema Matola.
Naye Kocha wa Mbeya City, Patrick Magata alisema licha ya kupata matokeo mabaya katika mechi tatu zilizopita, anaamini watakuwa wapinzani bora kwa Simba katika mtanange wa leo.
“Hatujapata ushindi katika mechi tatu zilizopita, licha ya kutokuwa na muda wa kutosha kujiandaa na mechi , lakini imani yetu ni kwamba tunakwenda kuwania pointi tatu na tunaamini tunaweza kuzipata,” alisema Magata.




