Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ameihakikishia Jumuiya ya Kimataifa kuwa, serikali imefungua milango kwa wawekezaji wenye nia ya kushirikiana na Tanzania katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya taifa.
Amesema kuwa, kwa zaidi ya miongo sita, Tanzania imeendeleza ushirikiano thabiti na wawekezaji na wadau wa maendeleo, huku ikiimarisha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara.
Rais Dk. Samia, alieleza hayo, alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mwenyekiti wa Biashara wa Jumuiya ya Madola na Baraza la Uwekezaji (CWEIC), Lord Hugo Swire, Ikulu jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, viongozi hao, walijadiliana kuhusu kuanzisha ushirikiano wa kibiashara na fursa za uwekezaji, zinazoweza kuchochea ukuaji wa uchumi na ajira nchini.
Rais Dk. Samia, alieleza kuwa serikali imefungua milango kwa wawekezaji wenye nia ya kushirikiana na Tanzania, kusukuma mbele ajenda ya maendeleo ya taifa na kuongeza kuwa, kwa zaidi ya miongo sita, nchi imeendeleza ushirikiano thabiti na wawekezaji pamoja na wadau wa maendeleo, huku ikiimarisha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara.
Akigusia matukio ya uvunjifu wa amani ya Oktoba 29, mwaka huu, Rais Samia, alisisitiza Tanzania inaendelea kuwa nchi yenye utulivu na ina mifumo madhubuti ya kushughulikia masuala yake ya ndani.
Aidha, aliihakikishia jumuiya ya wawekezaji kuwa, serikali itaendelea kuwajibika kwa usalama wa wawekezaji na biashara zao na kudokeza kuwa, nchi ipo katika hatua za awali za mchakato wa mapitio ya katiba unaokusudiwa kuimarisha utendaji wa taasisi na sekta ya biashara na uwekezaji.
Kwa upande wake, Lord Swire alionesha utayari wa CWEIC kuendeleza ushirikiano na Tanzania kama mshirika wa kimkakati kuvutia wawekezaji zaidi kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola.
Pia, alimshukuru Rais Dk. Samia kwa mapokezi na kumtakia kheri katika kuendeleza juhudi za kuimarisha uchumi wa nchi, huku akiiombea Tanzania kurejea katika hali ya utulivu.




