Na ATHNATH MKIRAMWENI
TANZANIA imetajwa kuwa moja ya nchi kinara barani Afrika katika mapambano dhidi ya Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa.
Hilo limebainishwa katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Kanda ya Afrika ya Wiki ya Kimataifa ya Uelewa wa Kudhibiti Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa (WAAW), uliofanywa na Makamu wa Rais, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Dk. Nchimbi, alisema Tanzania haijajipambanua tu kama mwenyeji wa tukio hilo barani Afrika, bali mshirika muhimu na kiongozi wa kimkakati katika kukabiliana na tishio hilo.
“Usugu wa dawa siyo jambo la baadaye, bali la sasa na matokeo yake, yanaonekana duniani kote, afya ya binadamu, wanyama, kilimo na mazingira, vimeunganishwa kwa karibu na tatizo hili, hivyo suluhisho lazima liwe la pamoja na sekta zote,”alisema.
Dk. Nchimbi, alieleza Tanzania imeweka UVIDA katika usimamizi wa kipaumbele cha taifa kwa kutekeleza Mpango wa Pili wa Taifa wa Kupambana na UVIDA (2023–2028) kupitia muunganiko wa sekta mbalimbali.
Alisema mpango huo, umeleta mafanikio makubwa ikiwemo kupungua kwa vifo, vinavyohusiana na UVIDA kwa asilimia 14.
Pia, alitaja kupungua kwa matumizi ya viuavijasumu nchini kwa asilimia 88 kama moja ya hatua za kihistoria zilizotambuliwa kimataifa na mchango wa Tanzania katika kushirikisha data za UVIDA katika majukwaa ya kikanda na kimataifa na kuongeza fedha za ndani kwa utekelezaji wa mpango huo.
Dk. Nchimbi, alisema katika kuongeza uelewa wa umma, Tanzania imeitafsiri rasmi dhana ya AMR kuwa Usugu wa Vimelea vya Magonjwa Dhidi ya Dawa (UVIDA) na imeendesha kampeni nyingi za kitaifa kuanzia ngazi ya juu hadi vijijini.
Aliitaja kampeni ya “Holelaholela Itakukosti” kama mfano bora uliotambuliwa na Afrika CDC, baada ya kufikia watu milioni 24.7.
Pia, alisema Tanzania imeanzisha ushirika wa wabunge wa kupambana na UVIDA, unaolenga kuimarisha nguvu ya kisheria, sera na ushirikiano kati ya watunga sera na wadau wa afya, mazingira, mifugo na kilimo.
Katika kukabiliana na maambukizi, alibainisha kuwa, utekelezaji wa kanuni za Kinga na Udhibiti wa Maambukizi (IPC), umeimarishwa, mifumo ya udhibiti wa usalama wa chakula, ukaguzi wa machinjio na chanjo za mifugo, imeongezwa kupunguza ueneaji wa maambukizi kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu.
Dk. Nchimbi, alieleza kuwa, upatikanaji wa dawa salama, umehakikishwa kupitia mfumo wa MSD na udhibiti wa TMDA, huku Sheria ya Afya kwa Wote, ikihakikisha wananchi wanapata huduma bora bila ubaguzi.
Makamu wa Rais, alisema Tanzania imepanda kutoka kiwango cha uwezo wa chini kabisa mwaka 2016 hadi viwango vya juu vya tatu na nne kwa mwaka 2024 katika utekelezaji wa mpango wake wa UVIDA, kiashiria cha dhamira, uthabiti na uwekezaji wa muda mrefu.
Alitaja maeneo sita ya vipaumbele ambayo Tanzania itaendelea kuyaboresha ambayo ni kuongeza uelewa wa umma, kuimarisha ufuatiliaji wa UVIDA, kupanua udhibiti wa maambukizi katika hospitali na mashamba, kusimamia matumizi bora ya dawa, kuimarisha udhibiti wa sheria na kuwekeza katika utafiti na ubunifu.
Aliwashukuru washirika wengine kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania katika mapambano hayo ya kimataifa dhidi ya usugu wa dawa na kusisitiza kuwa, hakuna nchi inayoweza kupambana na UVIDA peke yake.
Alisema ushirikiano wa kikanda na duniani ni muhimu katika kubadilishana taarifa, kuunganisha sera na kuimarisha mipango ya pamoja.
Aliisisitiza jamii kufuata matumizi sahihi ya dawa, kukamilisha dozi, kuepuka matumizi holela na kuzingatia usafi na kanuni za udhibiti wa maambukizi.
Vilevile alisema Tanzania itaendelea kujenga mifumo imara ya afya, kuwekeza katika utafiti wa kisayansi na kusimamia matumizi ya dawa kwa kuwajibika kulinda afya ya watu, wanyama na mazingira.
WAZIRI MCHENGERWA
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, alisisitiza umuhimu wa umoja wa kimataifa katika kupambana na tishio hilo linaloweza kudhoofisha matibabu ya kisasa.
Alisema Tanzania, ikiwa na mipango madhubuti ya kupambana na AMR, inaendelea kujizatiti katika kuimarisha mifumo ya afya kwa kuwekeza katika utafiti, kuimarisha mifumo ya udhibiti wa maambukizi na kuwajengea wananchi uelewa kuhusu matumizi sahihi ya dawa.



