Na ABDUL DUNIA
PAMOJA na kuanza vibaya katika kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) msimu huu, Simba bado ina nafasi ya kutinga robo fainali kama tu itachanga vyema karata zake kimahesabu katika mechi nne zilizobakia.
Wekundu hao wa Msimbazi waliopangwa kundi moja na Petro Atletico ya Angola, Esperance ya Tunisia na Stade Malien kutoka Mali, imeanza kwa vichapo katika mechi zake mbili ilizocheza.
Miamba hiyo yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam, ilianza kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Petro nyumbani kabla ya wiki iliyopita kukubali kipigo cha mabao 2-1 ilipochuana na Stade Malien ugenini.
Kutokana na matokeo hayo, sasa Simba ili kufufua matumaini yake ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo, inapaswa kuvuna angalau alama 10 au 12 katika mechi nne zilizobaki.
Katika mitanange iliyobakia itakayopigwa kuanzia Januari mwakani, Simba itacheza mara mbili na Esperance (nyumbani na ugenini), Petro ugenini kabla ya kumalizana na Stade Malien nyumbani.
Katika mchanganuo wa alama, ili Wekundu hao wa Msimbazi wafikishe alama 10 wanapaswa kushinda mechi tatu na kutoka sare moja kati ya mechi nne au kushinda zote ili kufikisha alama 12 ili kuwa na asilimia kubwa ya kucheza robo fainali ya michuano hiyo.
Tangu ilipofuzu hatua ya makundi ya CAFCL msimu wa 2018/2019, Simba haijawahi kushindwa kutinga robo fainali ya michuano hiyo kwa msimu wowote iliyotinga makundi.
Akizungumzia hali ya sasa ya kikosi chao, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema wana muda wa kutosha kujipanga kwa mechi zilizobaki kuhakikisha wanatinga robo fainali.
Ally alisema hadi kufikia katika mechi hizo, timu hiyo itakuwa imefanyiwa marekebisha makubwa kuhakikisha inatinga robo fainali ya michuano hiyo.
“Mechi yetu ya tatu ya hatua ya makundi tutacheza Januari 21, 2026 dhidi ya Esperance ugenini. Kutoka sasa hadi Januari 21 ni siku zaidi ya 50.
Katika siku hizo kikosi chetu kitafanyiwa mabadiliko makubwa ya kiufundi na itakapobidi kuongeza nguvu kwenye dirisha dogo tutafanya hivyo, na tunaamini mabadiliko hayo yataturejesha kwenye makali yetu,” alisema Ally.
Ally aliongeza kuwa: “Umefika ule wakati wa Simba yetu kuonesha maajabu yake na kuwashangaza watu, kwa sasa tunaanza maandalizi ya michezo yetu ya Ligi Kuu. Tukumbuke kuwa katika Ligi tuna mwenendo mzuri hivyo tunapaswa kuwekeza nguvu kubwa tusiteleze,” alisema.
Wekundu hao wa Msimbazi wameshinda mabao 3-0 dhidi ya Fountain Gate, 3-0 dhidi ya Namungo na 2-1 ilipochuana na JKT Tanzania.




