Happiness Mtweve
Dodoma
SERIKALI imesema imeshuhudia mapinduzi makubwa katika taasisi zinazohusika na utoaji wa haki baada ya kuanza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika Mahakama na Mabaraza ya Haki, hatua iliyochangia kuharakisha uendeshaji wa mashauri na kuongeza ufanisi katika utoaji wa haki.
Aidha, Serikali imesema kuwa chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kusisitiza utekelezaji wa mageuzi ya kidijitali kama nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa na uboreshaji wa huduma kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa jijini Dodoma leo Desemba 15, 2025 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angellah Kairuki, wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya TEHAMA kwa taasisi mbalimbali za kisheria.
Vifaa hivyo ni pamoja na kompyuta mpakato 70 na mashine za kuchapisha (printers) zilizogawiwa kwa Wizara ya Katiba na Sheria (10), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (20), Ofisi ya Mashtaka ya Taifa (20) pamoja na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Mahakama (20).
Waziri Kairuki amesema matumizi ya TEHAMA yameondoa urasimu, yameimarisha mifumo ya kazi, kupunguza msongamano wa mashauri na kuondoa mianya ya rushwa kwa watumishi wasio waaminifu.
Ameongeza kuwa teknolojia hiyo imewezesha pia kukubalika kwa ushahidi wa kielektroniki na kurahisisha tathmini ya utendaji wa Mahakama na watendaji wake.
“Hatua hizi zimewezekana kwa kiasi kikubwa kutokana na mchango wa Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutunga sera na sheria zinazowezesha utoaji wa haki kwa kutumia TEHAMA,” amesema Waziri Kairuki.
Ameitaja miongoni mwa sheria hizo kuwa ni Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015, Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya mwaka 2015 pamoja na Sheria ya Ushahidi ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007.




