• ePaper
Thursday, April 16, 2026
  • Login
No Result
View All Result
Uhuru Publication
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Hadithi
  • Login
No Result
View All Result
ePaper
Uhuru Publication
Home Habari

RAIS DK. SAMIA ATUMA UJUMBE WA AMANI

Abdurahman Jumanne by Abdurahman Jumanne
December 26, 2025
in Habari, Kitaifa
0
RAIS DK. SAMIA ATUMA UJUMBE WA AMANI
0
SHARES
6
VIEWS
Share on FacebookShare on Twitter

NA WAANDISHI WETU

UJUMBE wa amani, haki na utulivu umetawala katika salamu za Sikukuu ya Krismasi kutoka kwa viongozi mbalimbali, akiwemo Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambao wamesisitiza ndiyo msingi mkuu wakati huu ambao waumini wa dini ya Kikristro duniani wakiadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo.

Katika salamu zao, viongozi hao wamesisitiza kuwa wanadamu wanapaswa kuishi kwa kuilinda amani na kuwa mstari wa mbele kusisitiza haki na kukemea migogoro.

Akitoa salamu za sikukuu hiyo, Rais Dk. Samia alitoa wito kwa wananchi kusherehekea sikukuu hiyo kwa furaha na upendo.

“Ninawatakia kheri ya Sikukuu ya Krismasi Wakristo na Watanzania wote. Mnaposafiri kujumuika na ndugu, jamaa na marafiki katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, tusherehekee kwa furaha na upendo.

“Kuzaliwa kwa Yesu Kristo kutukumbushe upendo kwa Mwenyezi Mungu, upendo kwa kila mmoja wetu, wajibu wa kujitoa kuwasaidia wenye uhitaji, uvumilivu na unyenyekevu. Tuendelee kukumbuka wajibu wetu wa kutunza Taifa letu ili lidumu katika amani, utulivu, haki, ukweli na ustawi wa kila mmoja wetu sasa na vizazi vijavyo. Mwenyezi Mungu awabariki nyote,” alisisitiza Rais Dk. Samia.

SALAMU ZA PAPA LEO XIV

Kwa upande wake, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Leo XIV, alitoa wito wa kusitisha mapigano katika maeneo yenye migogoro duniani.

Papa Leo alisema watu wote wenye nia njema kuhakikisha Krismasi inakuwa siku ya amani na waonyeshe heshima katika siku hiyo ya kuzaliwa Yesu Kristo.

Baba Mtakatifu alisisitiza kuwa Sikukuu ya Krismasi ni mwaliko wa kutangaza na kushuhudia amani, umoja, upendo na mshikamano wenye udugu wa kibinadamu.

Aliwataka Wakristo kuishi kwa matumaini, kuendelea kuwa mashuhuda katika imani inayomwakilisha Yesu Kristo kupitia matendo ya huruma, kiroho na kimwili.

Papa Leo XIV aliongoza maadhimisho ya Sikukuu ya Krismasi katika Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

TUDUMISHE AMANI

Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Central Tanganyika, Dk. Dickson Chilongani, aliwasisitiza Watanzania kuendelea kudumisha amani huku akikemea tabia ya kutupiana lawama.

Dk. Chilongani alisema hayo jana jijini hapa alipohubiri katika ibada ya Sikuku ya Krismasi, iliyofanyika Kanisa la Roho Mtakatifu, Dayosisi ya Central Tanganyika.

Alisema vurugu zilizotokeza wakati wa uchaguzi mkuu mwaka huu, Watanzania hawajawahi kuishi maisha hayo, hivyo hategemei kuona yanajirudia tena kwani kila mtu anapaswa kulinda amani iliyopo nchini badala ya kuendelea kutupiana lawama.

“Mimi siku zile tatu ambazo watu walifungiwa ndani nilijaribu kutoka nje lakini, hali niliyoikuta sijawahi kuiona, nchi ilikuwa kimya sana hakuna watu mtaani, hakuna sauti za magari, mimi napenda sana kushinda shambani lakini kwa siku zile tatu ambazo tulizuiliwa ndani niliona kama mwaka,”alieleza.

MSISITIZO WA ASKOFU RUWA’ICHI

Askofu Mkuu wa Jimbo la Katoliki Dar es Salaam, Jude Thaddeus Ruwa’ichi, alisema ili amani iwepo lazima haki itendeke.

Akiwa katika ibada ya mkesha wa Krismasi, alisisitiza, “Amani na haki ni vitu viwili vinavyotengenezana na ni zawadi, wasifu unaofungamana na Kristo kwa hiyo wewe mkristo Mtanzania simama na yanayompendeza Mungu,”alisema Ruwa’ichi.

ASKOFU MOLLEL

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati, Dk. Godson Mollel, aliwataka wazazi na walezi kutumia sikukuu za mwisho wa mwaka vizuri.

Dk. Mollel aliyasema hayo jana alipotoa salamu za Sikukuu ya Krismasi katika Usharika wa Arusha Mjini, Kanisa Kuu  (Cathedral).

“Tunaomba Mungu leo siku ya amani katika familia, kweli ikawe amani, leo (jana) ni siku hata ya kubadilisha mlo jamani, tukale kwa furaha, siyo siku ya ujinga ni siku ya kufurahi na familia. Tunapokula tukumbuke Januari shule, tule kwa akili tuwapeleke watoto shule,” alisema Dk Mollel.

NENO LA RC CHALAMILA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alisema chuki ni miongoni mwa sababu kuu zinazosambaza uovu kwa kasi katika jamii, hivyo aliwataka waumini na Watanzania kuikataa chuki na kujinyenyekeza mbele za Mungu kupata msamaha wa kweli.

Chalamila aliyasema hayo aliposhiriki Ibada ya Sikukuu ya Krismasi iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Kimara Korogwe, Dar es Salaam, linaloongozwa na Mchungaji Wilbroad Mastai.

Alihimiza waumini kuendelea kujinyenyekeza mbele za Mungu ili kudumisha amani na usalama wa nchi, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.

Aliwataka wachungaji na viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa liendelee kudumisha amani, akibainisha kuwa palipo na amani ndipo maendeleo yanapopatikana.

TUSIMAMIE UKWELI

Akizungumza baada ya Misa Takatifu ya Krismasi, Paroko wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Yoseph, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padri Denis Wigira, alisema injili inafundisha kuwa, Yesu Kristo ni nuru halisi, hivyo jamii inapaswa kusimama katika ukweli.

“Nitoe wito kwa wananchi kutembea katika nuru kwa sababu anayetembea, anayesimama na anayeshuhudia katika ukweli basi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

“Niwaombe sana waumini wa dini ya Kikristo kutumia zawadi hii ya mtoto Yesu, itujaalie kutembea, kuupenda na kuusimamia ukweli kwa kila kitu tutakachokifanya kwa kuwa ukweli ni jambo muhimu na linapaswa kuzingatiwa,”alisema.

Paroko Denisi aliwashauri Watanzania kuendelea kudumisha amani ya nchi kwa kuwa amani ni tunda la haki.

TUTENDE MATENDO MEMA

Akizungumza katika mkesha wa misa  ya Krismas iliyofanyika Parokia ya Mtakatifu Yohane 23, Kimara Baruti, Dar es Salaam, Paroko wa Parokia hiyo, Padri Damas Nestory, alisema Yesu hakuzaliwa kufanya sherehe bali kumkomboa mwanadamu.

Paroko Nestory alisema kuzaliwa kwa Yesu kunaleta matumaini kwa wanadamu, hivyo wanatakiwa kutumia sikukuu hiyo kufanya mabadiliko ya kiroho kwa kufanya matendo yanayompendeza Mwenyezi Mungu.

Previous Post

SERIKALI YATOA MILIONI 800/- UJENZI KITUO CHA POLISI

Next Post

PM MWIGULU ASISITIZA USHIRIKIANO VIONGOZI WA DINI, SERIKALI 

Next Post
PM MWIGULU ASISITIZA USHIRIKIANO VIONGOZI WA DINI, SERIKALI 

PM MWIGULU ASISITIZA USHIRIKIANO VIONGOZI WA DINI, SERIKALI 

Leave a Reply Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Recommended

NI HESHIMA YA TANZANIA

NI HESHIMA YA TANZANIA

4 days ago
KAPOMBE, DUCHU WATOA MSIMAMO SIMBA

KAPOMBE, DUCHU WATOA MSIMAMO SIMBA

3 months ago

Popular News

  • PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    PROFESA IBRAHIM ATIA NENO TUME YA JAJI CHANDE

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SERIKALI YAFUTA LESENI 40 ZA UTAFITI  WA MADINI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • TIMU OFISI YA MAKAMU WA RAIS, WIZARA YA MAJI KUCHUANA MEI MOSI

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • SIMBA, FOUNTAIN GATE SIKU YA HESHIMA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0
  • RAIS DK. MWINYI AKAGUA MJI WA AFCON FUMBA

    0 shares
    Share 0 Tweet 0

Stay Update, Subscribe Now!

Check your inbox or spam folder to confirm your subscription.

Ukurasa Rasmi wa Televisheni ya Gazeti la Uhuru.

Facebook-f Instagram X-twitter Youtube tiktok
Quick Links
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalum
  • Kolamu
  • Makala
Services
  • ePaper
Contact Information
  • Dar es Salaam,Tanzania
  • info@upl.co.tz
  • +255 783 925 742
Uhuru Publications , 2025 © All Rights Reserved
  • Terms & Conditions
  • Privacy Policy
  • FAQ
No Result
View All Result
  • Home
  • Habari
  • Michezo
  • Uchaguzi
  • Burudani
  • Toleo Maalumu
  • Kolamu
  • Makala
  • Contact
  • Hadithi

© 2026 JNews - Premium WordPress news & magazine theme by Jegtheme.

Are you sure want to unlock this post?
Unlock left : 0
Are you sure want to cancel subscription?