Morogoro
NA LATIFA GANZEL
SERIKALI imetoa zaidi ya sh. milioni 800 kukamilisha ujenzi Kituo cha Polisi ngazi ya daraja B kilichopo Ifakara wilayani Kilombero mkoani Morogoro.
Akiweka jiwe la msingi katika kituo hicho kilichokamilika kwa zaidi ya asilimia 95, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Wakili Dustan Kyoba, alisema fedha hizo ni matokeo ya juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa usalama.
Wakili Kyoba alitoa shukran kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillus Wambura kwa kuungana na serikali kuchangia sh. milioni 32 kukamilisha mifumo ya Tehama katika kituo hicho.
Kyoba alisisitiza upandaji miti katika maeneo yanayozunguka kituo hicho na kuwekeza nguvu kuzuia uhalifu mtandaoni.
Kwa upande wake, Kamishina Msaidizi wa Polisi, Samuel Kijanga, alimshukuru mkuu huyo wa wilaya kwa kuhamasisha ujenzi huo.
Naye, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kilombero, SSP David Nkuba, alisema kituo hicho kimejengwa kwa ‘forced account’ ukisimamiwa na mkandarasi wa ndani.
Akizungumzia ujenzi huo, mkazi wa eneo hilo Laison Makwalilo alisema uwepo wa kituo hicho kitawezesha kupungua uhalifu katika wilaya hiyo.
Wakati huo huo, watu 14 wakiwemo wanaume 11 na wanawake watatu wamenusurika kifo katika ajali ya basi na lori iliyotokea juzi katika eneo la Magubike, Kata ya Magubike, Wilaya ya Kilosa barabara ya Morogoro-Dodoma huku chanzo cha ajali hiyo kikitajwa ni uzembe wa dereva wa basi
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, alisema ajali hiyo ilihusisha magari mawili yaliyogongana uso kwa uso ambapo gari la kwanza ni basi lenye namba za usajili T 577 DXL aina ya Yutong, mali ya Kampuni ya NASRI likiendeshwa na Alex Patric (40) mkazi wa Milandizi mkoani Pwani, likitokea Tarime kwenda Dar es Salaam.
Alisema gari la pili ni lori aina ya Scania lenye namba za usajili T 145 AFA na tela lenye namba T 148 AFK, mali ya Kampuni ya ATT, likiendeshwa na Robert Manunu (30) mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu likitokea Morogoro kwenda mkoani Tabora.
Majeruhi wa ajali hiyo walifikishwa katika Kituo cha Afya Magubike kupatiwa matibabu ambapo uchunguzi wa awali ulibaini chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa basi aliyetaka kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari. Kamanda huyo alisema dereva huyo wa basi anapatiwa matibabu chini ya ulinzi Jeshi la Polisi ili hatua zaidi za kisheria zichukuliwe.




