Na ZIANA BAKARI
BAADHI ya wataalamu wa saikolojia, wametaja mambo matatu yanayosababisha idadi kubwa ya wanaume, kuwa na hofu ya kuoa wanawake warembo katika jamii.
Mambo hayo matatu yaliyotajwa na wataalamu hao wa saikolojia ni athari za kisaikolojia, kijamii na kimtazamo ambazo husababisha wanaume kuwa na hofu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na UHURU, wanasaikolojia hao, walisema mwanaume anapaswa kujiamini anapotaka kuoa mwanamke mwenye mwonekano wa kuvutia katika jamii.
Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (TAPA), Albano Michael, alisema sababu za kisaikolojia zinatokana na mwanaume kutojiamini kupitia malezi na makuzi aliyowahi kupata nazo huchangia.
Alisema baadhi ya wanaume hujihisi kutokuwa na sifa ya kuoa mwanamke mwenye mwonekano wa kuvutia, kutokana na dhana binafsi na kuhisi hataweza kutoa huduma ipasavyo kutokana na mwonekano wake.
Alisema hali hiyo wakati mwingine, hutokana na historia ya nyuma ya mwanaume ambaye huenda aliwahi kukataliwa na wanawake wengi wenye mwonekano wa kuvutia.
Akizungumzia sababu za kijamii, Michael alisema sababu hizo, zinatokana na mazoea ya baadhi ya dhana zilizojengeka ndani ya jamii, mwanamke mwenye mwonekano wa kuvutia, hatadumu katika ndoa, jambo ambalo halina ukweli.
“Zipo baadhi ya jamii zinahisi kuoa mwanamke mwenye mwonekano wa kuvutia huaribu ndoa, kwa sababu, atawavutia wanaume wengi na kusababisha migogoro ya mara kwa mara, mwanaume hupata hofu na kuhisi kumpoteza mwanamke huyo,”alisema.
Pia, alisema sababu za kimtazamo binafsi, zinatokana na baadhi ya wanaume wanahisi wakioa wanawake wenye mwonekano wa kuvutia, watakuwa wasaliti kutokana na mvuto wao, hivyo hujawa hofu ya kuachwa, kujishusha thamani na kuona hawana vigezo vya kuwa nao katika ndoa.
“Wanaume wanapaswa kujua kuwa, mwanamke anatakiwa kuwa na tabia njema, nidhamu binafsi, mshirika mzuri wa mambo ya jamii na mwenye mtazamo chanya katika maisha, siyo mvuto pekee, hivyo, niwaombe wanaume, kuzingatia vigezo vilivyotajwa, wasiogope kuoa mwanamke mwenye mwonekano wa kuvutia kwa sababu, huongeza ladha ya upendo ndani ya ndoa,”alisema.
Mwenyekiti wa Kamati Endelevu ya Taaluma kutoka TAPA, Jesusa Malewo, aliwasihi wanaotaka kuoa kujua kuna suala la kuvumilia haiba ya mtu.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Saikolojia wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (DarTU), Dk. Hyasinta Kessy, alisema jambo muhimu kwa wanaume ni kuzingatia tabia njema, siyo mwonekano wa mwanamke.
Alisema haijalishi mwanamke au mwanaume ana mwonekano gani, jambo muhimu ni kuzingatia mtu mwenye tabia njema.
“Kipindi cha uchumba kinasaidia sana kusomana tabia na kujua namna ya kuishi na uliyemkusudia kumuoa, niwaombe tuzingatie sana tabia kwa sababu ni jambo muhimu na linapaswa kupewa kipaumbele,” alisema.




