Na NASRA KITANA
WAKATI Simba na Azam FC zikichuana katika dabi ya Mzizima, makocha Steve Barker na Florent Ibenge, wanatarajiwa kuwa na vita kubwa ya mbinu katika mtanange huo utakaopigwa leo visiwani Zanzibar.
Simba itachuana na Azam FC saa 2:15 usiku katika Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja katika mtanange wa nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026.
Wekundu hao wa Msimbazi wametinga nusu fainali baada ya kuongoza kundi C kwa alama sita wakati Azam FC ikishika nafasi ya kwanza kundi A kwa pointi saba.
Akizungumzia mchezo huo Kocha wa Simba, Barker raia wa Afrika Kusini, alisema amekiandaa vyema kikosi chake na ataingia na mbinu bora kuhakikisha wanashinda.
Muafrika Kusini huyo alikiri mtanange huo utakuwa mgumu lakini pia utakuwa muhimu kwa lengo la kuiimarisha timu yake.
“Ni mchezo muhimu kwetu kuhakikisha tunapata ushindi, najua tulipoteza mchezo wa mwisho, hivyo ninahitaji kukijenga kikosi chetu kiwe bora na chenye ushindani mkubwa tufunge magoli na kutinga fainali ili turudishe furaha ya Wanasimba,” alisema Barker.
Pia, Barker alisema mchezo huo utampa picha ya kujua ubora wa kikosi chake hivi sasa katika kucheza na timu kubwa hususan baada ya michuano hiyo watakabiliwa na michezo migumu katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia, Stade Malien ya Mali na Petro Atletico ya Angola.
Naye Kocha Ibenge alisema tayari amesuka mbinu bora kupata ushindi japokuwa wataingia katika mtanange huo kwa kuwaheshimu wapinzani wao.
“Ninaiheshimu Simba, ina kikosi kizuri lakini nitahakikisha tunaingia katika mchezo huo na mbinu za kushambulia zaidi tupate ushindi,” alisema.
Katika michuano hiyo, Simba ilishinda mechi zake mbili za kundi B wakati Azam FC ikishinda mbili na kutoka sare moja katika kundi A.
Simba ilishinda 1-0 dhidi ya Muembe Makumbi na 2-1 ilipocheza na Fufuni wakati Azam FC ikishinda 2-0 na Mlandege, 2-1 na URA na sare ya bao 1-1 ilipocheza na Singida Black Stars.




