NASRA KITANA na VICTOR MKUMBO
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema Tanzania imejipanga kuhakikisha michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027), inafanyika kwa ufanisi zaidi.
Tanzania inatarajia kuwa nchi mwenyeji wa michuano hiyo msimu ujao ikishirikiana na Kenya na Uganda.
Akizungumza katika hafla ya kuipongeza Taifa Stars, Ikulu, jijini Dar es Salaam, Rais Dk. Samia alimshukuru Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Dk.Patrice Motsepe, kwa kutambua mchango wa serikali katika kukuza soka nchini.
Rais Samia alifafanua, hiyo ni chachu ya kufanya maandalizi ya kina kuhakikisha fainali hizo zinafanyika kwa ufanisi zaidi msimu ujao.
Akidhidhirisha Tanzania imejipanga vema, alisema tayari miundombinu imeshaanza kukarabatiwa na viwanja vipya kujengwa, kuhakikisha michuano hiyo inafanyika nchini kama ilivyopangwa na maandalizi ya mapema yanahitajika ili kufanya vyema.
“Ninamshukuru Rais wa CAF, Motsepe kwa kunipatia tuzo kwa kutambua mchango wa serikali katika kukuza mchezo wa soka nchini, hii itakuwa chachu ya kujipanga na kuhakikisha michuano ya AFCON 2027 inafanyika kwa ufanisi zaidi,”alifafanua Rais.
Alisema alifuatilia michuano ya AFCON 2025, tangu ilipoanza msimu huu nchini Morocco na kuwapongeza wachezaji kwa kupambana na kufika hatua ya 16 bora.
Alisema wachezaji wote walishiriki michuano hiyo kwa nidhamu na mshikamano, kuhakikisha wanaitangaza zaidi nembo ya Tanzania.
Rais aliwapongeza wachezaji na benchi la ufundi la Taifa Stars, kwa kufika hatua ya 16 bora katika michuano ya AFCON msimu huu kwani wameipeperusha vyema bendera ya Tanzania.

Dk.Samia alisema hayo ni mafanikio makubwa na ushahidi tosha kwamba, mchezo wa soka Tanzania unapiga hatua kila wakati.
Kwa mujibu wa Rais Samia, alifuatilia michuano hiyo katika mechi zote ilipokuwa ikicheza Taifa Stars na kwamba, aliona juhudi za wachezaji wote walipokuwa uwanjani.
“Ninawapongeza kwa kufika hatua ya 16 bora, kwani ni mafanikio makubwa na ni ushahidi kuwa soka la Tanzania linapiga hatua.
“Nilifuatilia mechi zote na niliona matukio mbalimbali, yale yaliyotokea kwani tulicheza na wenyeji (Morocco) ni taifa lenye fedha, ni taifa lenye ushawishi kwa waandaaji,dunia imeona wazi kwamba Watanzania ni wapambanaji lakini ilibidi lile litokee, ninawapongeza sana kwani mmefanya kazi nzuri.
“Ninawapongeza wachezaji, benchi la ufundi na wanamichezo wote mliopo hapa, ni ukweli kwamba michezo yetu imepanda na inazidi kwenda juu.
“Aidha nizipongeze timu za taifa za kriketi kwa kufuzu Kombe la Dunia nchini Namibia, timu ya mpira wa miguu watoto wangu wanawake (Futsal), kwa kushiriki Kombe la Dunia nchini Ufilipino, ni hatua kubwa sana, hongereni sana.
“Pongezi zangu pia ziende kwa mabondia wetu waliotwaa mikanda ya kimataifa, ikiwemo timu ya Taifa ya Ngumi za Ridhaa iliyopata medali 18 ikiwemo moja ya dhahabu, fedha nne na 13 za shaba katika mashindano ya Kanda ya Tatu ya Afrika, yaliyofanyika Nairobi Kenya.
“Tunakwenda, tulipotoka siyo tulipo leo, jina la Tanzania linasikika, linaonekana katika kila fani, pia nawapongeza kwa walioshiriki mashindano ya Dunia yaliyofanyika Dubai ambayo bondia wetu alifika hatua ya 16 bora.
“Pia natoa pongezi kwa timu za taifa zilizofanya vizuri katika Ukanda wa CECAFA zikiwemo za vijana, shule kuogelea na timu za watu wenye ulemavu zote nazipongeza, zilibeba bendera na kuipeperusha vizuri nje ya Tanzania,”alisisitiza pongezi zake Rais Dk. Samia.
Rais Dk.Samia alisema kwa upande wa riadha anampongeza mwanariadha Alphonce Simbu, kwa kushinda medali ya dhahabu kwa mara ya kwanza katika mbio zilizofanyika Tokyo, Japan.
Pia alimpongeza Sisilia Ginoka Panga kwa kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya kilometa 15 zilizofanyikia nchini Brazil.
“Ninampongeza mwanariadha Simbu kwa kushinda medali ya dhahabu ya Tokyo Marathoni, vilevile nimpongeze kijana wetu Sisilia kwa kutwaa dhahabu ya mbio za kilometa 15, zilizofanyika Sao Paulo, Brazil kwa kutumia muda wa dakika 51:8, hawa ni Watanzania waliopeperusha bendera ya Tanzania katika riadha,” alisema Rais Dk. Samia.
Alilitaka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Baraza la Michezo la Taifa (BMT),kuwaandaa vyema vijana ambao wana vipaji kuzitumikia timu mbalimbali.
MOTISHA
Rais Dk.Samia alisema ameandaa mpango maalumu wa kutoa zawadi kwa wachezaji waliofanya vizuri na mgawo huo utatolewa kwa kada zote.
Alisema pia, amesikia maoni ya wachezaji kuhusu kuongezwa posho na hilo analishughulikia kuhakikisha timu zinafanya vizuri katika michuano mbalimbali.
“TFF na BMT mshirikiane kuendeleza vipaji vya vijana kuhakikisha wanakuwa katika kiwango bora na kuja kuzisaidia timu zetu na posho zao ziongezwe.
“Maandalizi hayawezi kufanyikiwa bila ushirikiano wa pamoja, niitake Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na wadau washirikiane kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.
“Pia sekta binafsi ziwekeze katika michezo kuhakikisha zinakuza vipaji kwa vijana kuanzia ngazi za chini.
“Tunapokwenda AFCON tuwe na mipango ya kuwanunulia tiketi wachezaji wanaofanya vizuri shuleni na kwenda kuwaangalia wale wa nje wanavyocheza, wajifunze kinachofanyika.
“Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayowezesha wanamichezo wetu kukuza na kuendeleza vipaji vyao, baadaye waje kutoa mchango wao katika timu za taifa,” alisema Rais Dk.Samia.
KABUDI AFUNGUKA
Waziri Mteule, Ofisi ya Rais, Ikulu, (Kazi Maalumu), aliyekuwa Waziri wa Michezo, Profesa Palamagamba Kabudi, alimshukuru Rais Dk.Samia kwa kumteua katika wizara hiyo kwani amekuwa mdau mkubwa wa michezo.
Profesa Kabudi alishukuru ushirikiano wa viongozi mbalimbali na kwamba, ataendelea kuwa mdau wa michezo huko anapokwenda katika majukumu yake mpaya.
“Ninakushuru Rais Dk.Samia kwa kuniteua katika wizara hii, kwani nimekuwa mdau mkubwa wa michezo, ninawashukuru viongozi walionipa ushirikiano kwa kipindi chote, hivyo ninaamini nitaendelea kuwa mdau wa michezo,”alisema Profesa Kabudi.
KARIA HUYU HAPA
Kwa upande wake Rais wa TFF, Wallace Karia alimshukuru Rais Dk. Samia, kwani serikali imeendelea kutoa sapoti ya kutosha katika michezo na kupiga hatua kubwa tofauti na ilivyokuwa awali.
Karia aliahidi makubwa zaidi katika michuano mbalimbali ikiwemo AFCON msimu ujao, kwani mpango wao ni kubeba kombe hilo.
“Ninakushukuru Rais Dk. Samia kwa sapoti serikali inayoendelea kutoa katika michezo, tunaahidi kufanya makubwa zaidi katika msimu ujao wa AFCON ikiwemo kubeba taji,”alisema Karia.





