Na NASRA KITANA
BAADA ya kufanikiwa kutinga fainali ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi, kocha wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema kuwa ana kazi kufanya kuhakikisha anaibuka na ushindi na kubeba taji la michuano hiyo mbele ya Azam FC.
Yanga na Azam zinatarajiwa kupepetana katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi, inayotarajiwa kufanyika kesho katika Uwanja wa Gombani, Pemba kuanzia saa 1:00 usiku.
Timu hiyo yenye maskani yake, Mtaa wa Twiga na Jangwani, Dar es Salaam, ilifanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kuifunga Singida Black Stars kwa bao 1-0, mchezo uliofanyika juzi Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja, visiwani Zanzibar.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Pedro alisema anawapongeza wachezaji wake, lakini bado ana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wanapata ushindi mnono katika mchezo wa fainali.
Alisema kuwa wachezaji wake walipambana kwa kiasi kikubwa kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo wa nusu fainali na hilo walifanikiwa.
Alisema malengo yake ni kubeba taji hilo msimu huu kutokana na kuwa na wachezaji wenye ubora wa hali ya juu.
“Mchezo wa fainali tutacheza na timu bora, nina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha tunafikia malengo tuliyojiwekea ya kuchukua ubingwa wa michuano ya msimu huu.
“Nitafanya uboreshaji wa baadhi ya maeneo kuhakikisha tunapata mabao mengi ya mapema na kujiwekea mazingira mazuri ya kubeba ubingwa,” alisema.
Kocha huyo alisema wachezaji wake wameendelea kuwa na muunganiko mzuri katika mechi zote walizocheza, ana imani watafanya vyema katika mchezo wa fainali.
Naye Kocha wa Singida Black Stars, David Ouma alisema kuwa mashindano ya Kombe la Mapinduzi ni mashindano mazuri kwa timu zinazoshiriki ili kujua mapungufu yao na kuyafanyia kazi.
Kocha huyo alisema ameona nini kinatakiwa kufanyika katika kikosi chake kuhakikisha kinakuwa na ubora zaidi kabla ya kurejea kwa michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Kwanza napenda kuwapongeza waandaaji wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi kwani yapo katika kipindi kizuri cha maandalizi kuelekea katika mashindano ya kimataifa na Ligi Kuu Bara, hivyo hiyo inatoa picha kwa benchi la ufundi kujua wapi kuna tatizo ili kufanya uboreshaji mapema na kuwa na kikosi imara zaidi,” alisema Ouma.
Kocha huyo alisema kuwa wamepoteza dhidi ya Yanga lakini anawapongeza wachezaji wake kwani wameonyesha kiwango kizuri katika mashindano hayo, ana imani anakwenda kurekebisha sehemu chache ili kuweza kuwa bora zaidi.
Yanga ilifanikiwa kutinga hatua nusu fainali baada ya kuongoza kundi C ikiinza kwa na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya KVZ na kuichapa bao 1-0 TRA huku Singida BS ikitinga nusu fainali baada ya ikishika nafasi ya pili ya kundi A baada ya kushinda mabao 3-1 dhidi ya Mlandege FC, sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC kabla ya sare ya 1-1 dhidi ya URA FC.




