Na AMINA KASHEBA
JASHO limemwagika. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema baada ya Yanga na Azam FC jana, kuonyesha moja kati ya fainali bora katika historia ya Kombe la Mapinduzi.
Katika fainali hiyo iliyopigwa Uwanja wa Gombani, Pemba, Yanga ilitwaa ubingwa kwa mikwaju ya penalti 5-4 kufuatia timu zote kumwaga jasho kwa zaidi ya dakika 120 bila ya kufungana.
Wakati kipa wa Azam FC, Aishi Manula, akionyesha umahiri mkubwa katika dakika 120, kipa wa Yanga, Abubakar Mshery aligeuka shujaa wa timu yake baada ya kuokoa mkwaju wa penalti ulioipa ushindi miamba hiyo.
Wachezaji wa Yanga waliofunga penalti ni Emmanuel Mwanengo, Prince Dube, Pacome Zouzoua, Mudathir Yahya na Bakari Mwamnyeto.
Wakati mkwaju wa penalti wa Landry Zouzou ukidakwa na Mshery, nyota wa Azam FC walioweka kimiani mikwaju hiyo ni Yahya Zayd, Sadio Kanoute, Twalibu Nuru na Kamanya.
Katika dakika 90, timu zote zilishambuliana kwa zamu huku makipa wa timu zote wakionyesha umahiri wa kuzuia michomo mbalimbali.
Hata hivyo, dakika ya 72, nyota wa Azam FC, Cheickna Diakite alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano.
Licha ya kuwa pungufu, Azam FC iliendelea kuwa na utulivu katika eneo la ulinzi hatua ambayo iliifanya Yanga kuwa na wakati mgumu wa kupata bao.
Baada ya dakika 90 kumalizika, timu hizo ziliongezewa dakika 30, ambapo katika dakika ya 114, Yanga ilipata penalti baada ya beki wa Azam FC, Twalibu Nuru, kuushika mpira ndani ya eneo la hatari katika harakati za kutaka kuokoa mpira.
Hata hivyo, kipa Aishi Manula aliendelea kuibakisha Azam FC mchezoni baada ya kuokoa penalti hiyo iliyopigwa na staa Pacome Zouzoua dakika ya 115.
Azam FC: Aisha Manula, Nathaniel Chilambo, Landry Zouzou, Lameck Lawi, Twalib Nuru, Himid Mao/ Sadio Kanoute, Zidane Sereri, Feisal Athuman, Jephet Kitambala/ Yoro Diaby , James Akaminko/ Yahya Zayd na Cheickna Diakite.
Yanga: Abuutwalib Mshery, Kibwana Shomary/ Bakari Mwanyeto, Chadrack Boka/Mohamed Hussein. Dickson Job, Ibrahim Bacca, Moussa Bala Conte, Maxi Nzengeli/ Sheikhan Abdallah, Duke Abuya/ Mudathir Yahya, Prince Dube, Pacome Zouzou na Celestin Ecua/Edmund John/ Emmanuel Mwanengo.




