Na Hamis Shimye
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuwa kiongozi wa mfano na mwenye kuwajibika kwa Watanzania kutokana na ubunifu, uweledi na usimamizi madhubuti wa mifumo ya kifedha.
Kuondolewa kwa Tanzania katika orodha ya nchi zilizo na hatari kubwa kifedha na Jumuiya ya Nchi za Ulaya ni heshima kubwa kwa nchi na kiongozi wake. Hii inatokana na kitendo hicho kusaidia kuonyesha uaminifu, uadilifu wa sekta ya fedha kimataifa.
Pia, hii ni ishara ya uaminifu kuondolewa katika orodha hiyo, ni hatua inayofahamika kimataifa kama sehemu ya uwepo wa ufanisi wa mfumo wa kupambana na utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi.
Uamuzi wa EU unajumuisha nchi sita za Afrika, ikiwemo Tanzania, baada ya nchi hizo kukidhi viwango vya kimataifa vya kupambana na uhalifu wa kifedha, inatarajiwa kuongeza uaminifu wa mfumo wa kifedha kwa nchi.
KItendo hicho kinasaidia kuweka chachu ya maendeleo ya uwekezaji Tanzania ambapo wawekezaji wa kigeni ni wakati mwafaka wa kuja kuwekeza kutokana na uwepo wa usalama wa fedha zao, kupungua kwa gharama na ugumu wa miamala ya kimataifa.
RAIS SAMIA BINGWA WA MAGEUZI YA SEKTA YA FEDHA
Rais Dk. Samia amekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio haya ya Tanzania kuondolewa katika orodha ya nchi hatarishi kifedha ya Umoja wa Ulaya (EU) kutokaa na mikakati mbalimbali.
Mchango wake unaonekana katika maeneo mbalimbali, hususan katika uongozi wa kisiasa na kiutawala, ambapo amekuwa kiongozi mwenye kujitolea katika kuboresha utawala wa sheria na kudhibiti vitendo vya uhalifu wa kifedha.
Uongozi wa Kisiasa katika Kupambana na Uhalifu wa Kifedha
Kuongeza juhudi za udhibiti wa utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi: Rais Samia ameweka mkazo mkubwa katika kuboresha mifumo ya kifedha na udhibiti wa fedha, kwa kushirikiana na taasisi za kimataifa ikiwemo FATF (Financial Action Task Force).
Hii ilitokana na Tanzania kuboresha sheria na kanuni zinazohusiana na utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi, na kufanya mabadiliko katika mifumo ya udhibiti wa fedha na kuleta mafanikio makubwa.
Pia, amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha ushirikiano na taasisi za kimataifa kwa serikali kuendelea kujenga na kuimarisha uhusiano na taasisi za kimataifa, kama vile EU na FATF, ili kuhakikisha Tanzania inatambuliwa kama nchi inayozingatia sheria na inayofuata viwango vya kimataifa vya udhibiti wa kifedha.
MAGEUZI YA KIUCHUMI NA KIFEDHA
Rais Samia ameanzisha mageuzi mbalimbali katika sekta ya kifedha, ikiwa ni pamoja na kuboresha mifumo ya upokeaji na usimamizi wa fedha za kigeni, kuimarisha usalama wa mifumo ya benki, na kuanzisha mikakati ya kupambana na vitendo vya uhalifu wa kifedha.
Uboreshaji wa mifumo ya kifedha umesaidia kuboresha mazingira ya biashara. Rais Samia amekuwa akisisitiza mazingira bora ya biashara, kwa kuondoa vikwazo na kuhamasisha uwekezaji kutoka nje.
Uamuzi wa kuondoa vikwazo vya kifedha na kuhakikisha miamala ya kifedha kati ya Tanzania na nchi za Ulaya inakuwa rahisi zaidi ni sehemu ya mageuzi ya kisera yaliyofanywa chini ya utawala wake.
USHIRIKIANO NA NCHI NYINGINE ZA AFRIKA
Kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa: Rais Samia ameendelea kutafuta ushirikiano wa kimataifa na wa kikanda ili kuhakikisha kuwa Tanzania inaungana na mataifa mengine katika juhudi za kupambana na vitendo vya kifedha haramu.
Hii imekuwa na matokeo chanya kwa Tanzania kuondolewa katika orodha ya nchi hatarishi kifedha na kuimarisha nafasi yake katika soko la kimataifa ambalo kwa miongo kadhaa imekuwa imara na yenye mafanikio makubwa kimataifa.
KUHAMASISHA UWEKEZAJI WA KIMATAIFA
Kufungua fursa za uwekezaji: Kuondolewa kwa Tanzania katika orodha ya nchi hatarishi kifedha, Rais Samia ameweka mazingira ya kuvutia kwa wawekezaji wa kimataifa.
Hii ni muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania na kukuza sekta za viwanda, miundombinu, biashara. Rais Samia amechukua hatua madhubuti na kuonyesha uongozi wa kimkakati katika kuhakikisha nchi inaendelea na mageuzi ya kifedha na kisheria.
Ili nchi kuwa salama na ya kuvutia kwa uwekezaji wa kimataifa. Hii ni hatua muhimu katika kuimarisha uchumi na nafasi ya Tanzania katika medani za kimataifa na kusaidia kuleta mabadiliko kwa sekta nyingine.
Rais Samia amekuwa na nafasi nzuri ya kuleta mabadiliko zaidi katika sekta nyingine za uchumi, hasa katika maeneo ambayo yamekuwa na mchango wa kukuza maendeleo ya nchi kwa muda mrefu.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA
Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Deogratius Luswetura, alipongeza na kuiagiza Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuongeza udhibiti wa sekta ya fedha ili kuwalinda wananchi dhidi ya taasisi zisizo rasmi zinazotoa mikopo umiza, maarufu kama “Kausha Damu”, ambayo imekuwa ikisababisha watu kupoteza mali zao.
IMANI YA KIMATAIFA NA FATF
Naibu Waziri alisema kuondolewa kwa Tanzania katika orodha hiyo (baada ya kuondolewa pia katika FATF Grey List mwishoni mwa 2025), kutarahisisha miamala ya kifedha kati ya Tanzania na nchi za Ulaya kuanzia Januari 29, 2026.
“Hatua hii inafungua milango mipya ya uwekezaji, inaongeza ushindani wa bidhaa zetu kimataifa na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu salama cha biashara barani Afrika,” alisema Naibu Waziri.
GREY LIST NI NINI?
Grey list ni orodha ya nchi ambazo zilikuwa na mapungufu katika kudhibiti uhalifu wa kifedha ikiwemo utakatishaji wa fedha (money laundering), ufadhili wa ugaidi ambapo Tanzania imekuwa mstari wa mbele kuondokana na hali hiyo.
Tanzania imeondolewa katika orodha ya maeneo yaliyo katika hatari kifedha, hasa kwenye listi za kimataifa zinazohusiana na udhibiti wa uhalifu wa kifedha, uondoaji wa pesa haramu (money laundering) na ufadhili wa ugaidi.
Juni 2025, Financial Action Task Force (FATF) taasisi ya kimataifa inayoongoza kukabiliana na uhalifu wa kifedha ilitangaza Tanzania imeondolewa katika “grey list” (orodha ya nchi zilizo chini ya ufuatiliaji wa juu kwa sababu ya upungufu kwenye mifumo ya kupambana na utakatishaji wa fedha na ufadhili wa ugaidi).
Hii ilifanyika baada ya nchi kutimiza vigezo vya kimataifa na kufanya mageuzi makubwa katika sheria na taasisi zake za kifedha. Kuondolewa huko inaashiri Tanzania imeboresha mifumo yake ya kupambana na uhalifu wa kifedha.
Mafanikio haya yanaongeza imani ya wawekezaji wa kimataifa, kurahisisha shughuli za kifedha za kimataifa, na kupunguza gharama/masharti ya ukaguzi wa miamala ya kifedha.
Tanzania kupata mafanikio haya makubwa kwa kuondolewa rasmi katika orodha za mataifa yenye mifumo hatarishi ya kifedha, hatua inayoongeza imani ya wawekezaji na kurahisisha miamala ya kimataifa.
HATUA ZILIZOFANYIKA
Juni 13, Tanzania kuondolewa katika Orodha ya Kijivu ya FATF, Kikosi Kazi cha Kifedha cha Kimataifa (FATF) kiliiondoa Tanzania kwenye “Orodha ya Kijivu” (Grey List). Tanzania ilikuwa imewekwa chini ya ufuatiliaji tangu Oktoba 2022 kutokana na upungufu katika kupambana na utakatishaji fedha na ufadhili wa ugaidi.
Pia, Tanzania iliondolewa katika Orodha ya Umoja wa Ulaya (EU): Kufuatia hatua ya FATF, Umoja wa Ulaya uliiondoa rasmi Tanzania katika orodha yake ya nchi za tatu zenye hatari kubwa (High-Risk Third Countries) kufikia Januari 2026.
Hatua hiyo inamaanisha kuwa miamala ya kifedha kati ya Tanzania na nchi za Ulaya haitafanyiwa ukaguzi wa ziada uliokuwa unachelewesha biashara.
Tanzania imefanya mageuzi ya kisheria na kitaasisi, ikiwemo kuimarisha sheria ya kuzuia utakatishaji fedha na kuongeza ufanisi wa Kitengo cha Ujasusi wa Fedha (FIU) katika kusimamia sekta ya fedha.
Faida kwa Taifa
Kupungua kwa gharama na muda wa kufanya miamala ya kimataifa. Kuongezeka kwa imani ya wawekezaji wa kigeni na fursa za mikopo nafuu. Kuimarika kwa sifa ya nchi katika mifumo ya kifedha ya kimataifa.




