Na NASRA KITANA
UNAWEZA kusema ni mechi ya hesabu ambapo Simba itashuka dimba la Stade Olympique Hammadi nchini Tunisia kupambana na Esperance De Tunis.
Pambano hilo la Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi, limepangwa kuanza kufanyika saa 1:00 usiku, kocha wa timu hiyo, Steven Barker, alisema mechi hiyo ni kama fainali hivyo watapambana kuhakikisha wanapata ushindi.
Wekundu wa Msimbazi wataingia uwanjani huku wakipiga hesabu kali kuhakikisha wanachukua pointi tatu baada ya kucheza mechi mbili za michuano hiyo na kupoteza na kusababisha kuburuza mkia katika kundi hilo.
Simba inapiga hesabu hizo, kuhakikisha inasonga mbele baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Stade Malien ya Mali mabao 2-1 kabla ya kupokea kichapo kingine cha bao 1-0 kutoka kwa Petro Atletico ya Angola.
Huku Esperance nao wakipiga hesabu baada ya kucheza mechi mbili ambapo zote imetoka sare katika michuano hiyo yenye ushindani mkubwa na hivi sasa, timu hiyo ipo nafasi ya tatu katika kundi hilo.
Esperance ilianza kutoka sare ya 1-1 na timu ya Petro Atletico ya Angola na kisha ilitoka suluhu na Stade Malien katika ligi hiyo ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya makundi.
KOCHA WA SIMBA
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Barker alisema kuwa kila mchezo kwao ni kama fainali hivyo wataingia katika mchezo huo kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
Alisema katika kundi lao hawajapata ushindi katika mchezo wowote ule hivyo huo ni mchezo wao muhimu wa kupata matokeo ili kujizolea pointi tatu muhimu.
“Tunaingia katika mchezo huo tukiwa tunahitaji kupata ushindi, utakuwa mchezo mgumu na wenye changamoto kubwa lakini hatutakubali kuona tunapoteza, lengo letu ni kupata pointi tatu muhimu,” alisema Barker.
Kocha huyo alisema kuwa watawaheshimu wapinzani wao kwako wapo ugenini lakini hawata waogopa kwani anaimani kubwa na kikosi chake kuwa kitafanya vizuri.
Barker alisema kuwa mashabiki na wapenzi wa timu hiyo waendelee kuipa sapoti ya kutosha timu hiyo ili iweze kufanya vizuri na kuwaongezea morari wachezaji wao ili waweze kupata matokeo mazuri.
KAULI YA WACHEZAJI
Akizungumza kwa niafa ya wachezaji wenzake wa Simba, Rushine De Reuck alisema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanatumia vyema mbinu walizopewa na kocha wao kupata ushindi.
“Ni mchezo mgumu kwetu tutaingia kwa kuwaheshimu wapinzani wetu na kutafuta matokeo ya mapema, hatutakubali kupoteza, mwalimu wetu amerekebisha mapungufu yote yaliojitokeza katika mechi zilizopita,” alisema.
Rushine alisema kuwa haijalishi wapo katika uwanja wa ugenini, wamejipanga kujitoa kwa jasho na damu kuhakikisha wanapata ushindi wa pointi tatu muhimu.
Nyota huyo alisema wachezaji wote wana morari ya kutosha kuhakikisha wanashinda mchezo huo ambao ni muhimu kwao kupata ushindi.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Ahmed Ally alisema huo ni mchezo wa kufa au kupona hivyo wachezaji wameapa kufia uwanjani.
“Tunaomba Watanzania na wapenzi wa soka wote waweze kuiombea timu yetu ili iweze kufanya vizuri katika mchezo wetu muhimu ambao ni lazima kushinda ili tupate pointi tatu,” alisema Ahmed.
Katika mchezo wa leo, timu ya Espérance de Tunis itamkosa Nahodha wao, Yacine Meriah katika mchezo wa leo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Simba.
Yacine Meriah anakabiliwa na tatizo la misuli alilopata mapema mwezi huu.




