Na SUPERIUS ERNEST
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuandika historia kila kukicha kupitia uzinduzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Rais Dk. Samia, ameandika historia nyingine baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa matanki 15 ya mafuta wenye thamani ya sh. bilioni 678, hafla iliyofanyika Kigamboni Dar es Salaam, huku akisisitiza kuwa uwekezaji huo ni wenye tija katika kukuza uchumi.
Pia amesema mradi huo utaimarisha usalama wa nchi katika sekta ya mafuta ambayo ni nyenzo kubwa kwa maendeleo ya kiuchumi.
Amesema uwekezaji huo ni wa kimkakati katika kuimarisha uwekezaji kuwa kitovu cha kati cha uwekezaji kikanda na kimataifa.
Akifafanua kuhusu tija ya uwekezaji huo, amesema utasaidia katika kuchochea maendeleo kupitia uhifadhi wa mafuta na kuimarisha usalama wa nchi.
Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kupitia ahadi alizoahidi katika uchaguzi mkuu hususan kuongeza uwekezaji na kuboresha uwezo wa kuhifadhi mafuta kwa njia ya kisasa kwa lengo la kukuza uchumi.
Ametaja faida za uwekezaji huo, ni kusaidia taifa hususan kipindi inapotokea mabadiliko na migogoro ya kidunia kama ile inayoendelea sasa Mashariki ya Kati, kuepuka athari kubwa zaidi hasa kupanda kwa bei ya mafuta.
“Kama tunavyoshuhudia changamoto za kidunia zilizopo sasa zimesabababisha upandaji wa bei ya mafuta kwa siku za hivi karibuni, sasa hatujui itakuwaje kadiri siku zinavyokwenda, hivyo mradi huu ni muhimu kutusaidia kuwa na akiba ya kutosha ya mafuta katika vipindi kama hivi,” amesema.
Amesisitiza katika kuhakikisha mifumo ya serikali ya utoaji huduma inasoma na kuwepo uwazi katika usimamiaji wa miradi ya kimkakati ukiwemo huo.

“Niwasisitize wakandarasi kuhakikisha wanasimamia vyema ujenzi wa mradi, ujengwe kwa ufanisi mkubwa na ukamilike kwa wakati,” amesema.
Amesema matarajio yake ni kwamba mradi huo utajengwa kwa ufanisi na kukamilika kwa wakati kama ulivyopanga, atauzindua mwakani.
Kuhusu maboresho ya bandari, Rais Dk. Samia, amesema Dar es Salaam ina mchango mkubwa kiuchumi, kupitia uwekezaji mkubwa uliofanyika kushirikiana na sekta binafsi, hivyo mradi huo utaongeza ukuaji wa uwekezaji bandarini.
Kwa mujibu wa Rais Dk. Samia maboresho makubwa ya uwekezaji yaliyofanyika ikiwemo miundombinu ya barabara na nyinginezo, yamewezesha bandari hiyo kuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa zikiwemo za mafuta ambazo zimekuwa zikitua katika bandari zingine kubwa za kimataifa.
Amefafanua kwamba pamoja na uwekezaji mkubwa wa bandari ya Dar es Salaam na ule unaotarajiwa kufanyika Bagamoyo, utawezesha Tanzania kupokea meli zenye ukubwa wa aina yoyote bila kikwazo.
Ameeleza kwamba uwekezaji huo umesaidia katika kuongeza mapato tangu kuanza, ikiwemo kodi ya forodha.
Kimsingi amesema uamuzi wa uwekezaji ambao ulifanywa na serikali ulikuwa ni wa faida na kimkakati kuhakikisha taifa linakua kiuchumi.
Rais Dk. Samia amesema kupitia maboresho hayo bandari imeongeza ufanisi mkubwa wa kuhudumia wateja mbalimbali na kuongeza mapato.
Awali akimkaribisha Rais Dk. Samia, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amemshukuru kwa kukubali kuweka jiwe la msingi katika mradi huo huku akieleza utakavyochochea ukuaji uchumi.
Amesema mradi huo utakuwa mchango mkubwa wa kiuchumi na kuongeza upanuzi wa matumizi ya bandari na wigo wa usafirishaji wa shehena hata zile za mataifa mbalimbali.
Amesema hatua hiyo ni umuhimu katika ukuaji uchumi kupitia usafirishii wa mafuta, ambayo ni msingi mkubwa wa maendeleo ya maisha ya kila siku ya wananchi.
Amesema wamejipanga vyema kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa ufanisi mkubwa na kukamilika kwa wakati uliopangwa.
Profesa Mbarawa amempongeza Rais Dk. Samia kwa uwekezaji wa kisasa wa bandari, ambao umeendelea kutoa tija huku akisema wizara inaendelea na usimamizi wa ujenzi na upanuzi wa gati zingine.
Profesa Mbarawa amesema mradi huo ni sehemu ya mpango wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam, unaolenga kuongeza ufanisi, ushindani na mchango katika uchumi wa taifa.
Amesema matenki hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi meta za ujazo 378,000 za mafuta na yatapunguza muda wa meli za mafuta kukaa bandarini kutoka wastani wa siku 10 hadi tatu, hatua itakayoongeza ufanisi, kuvutia wawekezaji na kuimarisha usalama wa nishati.
Kwa mujibu wa Profesa Mbarawa, mradi huo unakwenda sanjari na ujenzi wa magati mapya yenye urefu wa meta 500 kila moja, yakitarajiwa kuongeza uwezo wa bandari hadi kufikia kuhudumia tani milioni 60 kwa mwaka.
Waziri huyo amesema katika kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka jana, Bandari ya Dar es Salaam ilihudumia tani milioni 19.9 za mizigo, huku serikali ikilenga kufikia tani milioni 40 ifikapo mwaka wa fedha 2025/26.
Profesa Mbarawa amesema uboreshaji huo unaendana na mkakati wa kuimarisha usafirishaji wa mizigo kupitia Reli ya Kisasa (SGR), kupunguza utegemezi wa barabara na kuongeza ufanisi wa usafirishaji ndani na nje ya nchi.
Waziri huyo alitoa rai kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na viunga vyake na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi katika tukio hilo kubwa na la kihistoria kwa nchi.
Amefafanua kuwa katika kuendelea kupunguza msongamano wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam wameendelea kujenga bandari kavu mbalimbali, ikiwemo Kwala ambazo zimekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza ufanisi na kukuza uchumi.
Amempongeza Rais Dk. Samia kwa mageuzi makubwa ya Bandari ambayo ameyafanya kupitia uwekezaji wa kimataifa, hali ambayo imeendelea kuchochea kasi ya ukuaji uchumi.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk. Rose Migiro, Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Stanley Mkandawile, amempongeza Rais Dk. Samia kwa kuendelea kutekeleza mradi huo kwa kasi kubwa, huku akisema ukikamilika utasaidia kupungua kwa gharama za mafuta.
“Kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi tunakupongeza kwa mradi huu mkubwa, siyo huu tu, kwa utekelezaji wa miradi mingine mikubwa inayoendelea kutekelezwa ndani ya nchi yetu, mkoa wetu na wilaya yetu ya Kigamboni, kwani barabara nyingi zilizokuwa zimeshindikana zinajengwa sasa katika kipindi chako,”amesema.
Akiwasilisha salamu za pongezi za wabunge, Spika wa Bunge, Mussa Zungu, amempongeza Rais Samia kwa jitihada zake za kuhakikisha changamoto za kidunia zilizopo kwa sasa haziathiri uchumi wa taifa.

Spika Zungu alisema kupitia uwekezaji huo, utasaidia kuhudumia mataifa yaliyozunguka Tanzania katika kukabiliana na changamoto za kidunia zilizopo.
Aliwasisitiza wananchi kuelewa kuwa uwekezaji huo ni kwa manufaa ya wananchi siyo viongozi au taifa lingine hivyo waunge mkono.
Aidha alisema Rais Dk. Samia amefanya kazi kubwa ya kuongeza kiwango cha ukuaji uchumi tangu aingie madarakani, hivyo kila mwaka kiwango cha ukuaji uchumi kimekuwa kinaongezeka kutokana na dhamira na jitihada zake za dhati.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila alisema mradi huo unaakisi maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja, kwani katika utekelezaji wa shughuli zao lazima watumie usafiri na usafirishaji ambao uhitaji mafuta katika vyombo vya usafiri.
“Ujenzi wa matenki haya ni kichocheo cha kuunganisha uchumi na kutatua changamoto za ndani za nishati za ndani na nje ya nchi, kwa sababu ya umuhimu wa Tanzania katika kufungua uchumi wa mataifa mengine kupitia Bandari ya Dar es Salaam,” alisema.
Chalamila alisema utekelezaji wa mradi huo ni kichocheo cha miradi mingine hususan barabara, madaraja ambayo yalikuwa changamoto kubwa katika wilaya na mkoa huo, huku akimpongeza Waziri wa Ujenzi kwa kazi hiyo kubwa.
Alisema ujenzi wa barabara mbalimbali Kigamboni unaakisi kazi kubwa anayoifanya Rais Dk. Samia katika mkoa wa Dar es Salaam.
Mtendaji Mkuu wa Bandari TPA, Plasduce Mbossa alisema kuwa mradi huo wenye thamani ya sh. bilioni 678 ni wa kihistoria na kimkakati wenye tija kubwa kiuchumi.
Alisema ujenzi wa matanki hayo utasaidia kupunguza gharama na kuimarisha usalama wa kiuchumi kwani utaepusha kusubiri meli zishushe mafuta bali nchi itakuwa na akiba ya kutosha hata pale inapotokea changamoto za kidunia.
Alisema pia utaongeza ushindani katika Bandari ya Dar es Salaam kwa kuepusha msongamano mkubwa wa meli za mafuta bandarini na kuvutia zaidi wafanyabiashara wa mafuta wa mataifa mengine kutumia bandari hiyo.




