Na MWANDISHI MAALUMU
WATOTO 15 wenye matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ikiwemo matundu kwenye moyo na mishipa ya damu ya moyo kutokuwa katika mpangilio wake wa kawaida, wamefanyiwa upasuaji katika kambi maalumu ya siku tano iliyofanyika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Kambi hiyo iliyomalizika jana chini ya uratibu wa msanii wa muziki wa Bongo Fleva, Ben Paul, ilifanyika kwa kushirikisha wataalamu wa JKCI na wenzao kutoka taasisi isiyo ya kiserikali ya Moyo Mission ya nchini Ujerumani.
Akizungumza kuhusu kambi hiyo, Mkurugenzi wa Upasuaji wa Moyo wa JKCI, Dk. Angela Muhozya alisema ushirikiano kati ya JKCI na Moyo Mission katika kutoa huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto umekuwa wa mafanikio makubwa kutokana na uzoefu na uwezo walionao watalamu hao kutoka Ujerumani.
“Tunaishukuru serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuruhusu timu ya wataalamu wanne kutoka Ujerumani wakiwemo madaktari bingwa wawili wa upasuaji wa moyo, mtaalamu mmoja wa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) pamoja na mtaalamu wa mitambo ya mapafu kuja JKCI kuongeza nguvu,” alisema Dk. Angela.
Alisema ushirikiano kati ya JKCI na Moyo Mission wa kwanza kufanyika ambapo watalaamu hao, pia walipata fursa ya kubadilishana uzoefu wa kitaalamu na kujifunza mbinu za kitabibu.
“Tunashukuru kwani watoto wa kitanzania wamenufaika na kambi hii, pia JKCI tumefaidika kwa kupata vifaatiba vya kisasa kwa gharama naafuu kutokana na washirika wetu kuwa karibu na kampuni zinazotengeneza vifaa vya matibabu ya magonjwa ya moyo,” alisema Dk. Angela.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chuo cha Heart Center kilichopo Hamburg Ujerumani ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji moyo kwa watoto, Dk. Daniel Biermann alisema wamechagua kushirikiana na JKCI kutokana na taasisi hiyo kuwa na miundombinu bora inayowawezesha kutoa huduma za kibingwa kwa ufanisi.
“Mazingira mazuri yamechangia kufanikisha upasuaji wa moyo kwa watoto na tunatarajia kuendeleza ushirikiano huu kwa muda mrefu na tunapanga kuja zaidi ya mara mbili kwa mwaka kuwasaidia watoto wa Kitanzania kupata matibabu na kuokoa maisha yao,”alisema Dk. Biermann.
Naye, Mratibu wa ushirikiano huo kutoka Ujerumani, Marie Biermann alisema lengo ni kuwajengea uwezo watalaamu wa ndani kupitia mafunzo yatakayowasaidia kujiendeleza kitalaamu katika masuala ya matibabu ya magonjwa ya moyo.
“Taasisi hii ina wataalamu wenye uwezo mkubwa katika matibabu ya magonjwa ya moyo kwa watoto, hivyo kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo zaidi waendelee kutoa huduma za kibingwa na bobezi” alisema Marie.
Mmoja wa mzazi ambaye mtoto wake alifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu kwenye moyo katika kambi hiyo, Nyaboke Korosso aliwashukuru watalaamu wa afya waliofanya upasuaji huo kwa mafanikio na kuokoa maisha ya mtoto wake.
Kupitia kambi hiyo watoto hao wamapata huduma za kibingwa za upasuaji hatua inayosaidia kurekebisha matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo na kuwapa nafasi ya kuishi maisha yenye afya bora.




