Na NASRA KITANA
WAKATI Azam ikitarajia kuikabili Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara leo, mechi hiyo inatarajiwa kuwa ya kisasi na heshima.
Katika mchezo huo, Azam itahitaji ushindi ili kulipa kisasi cha kufungwa mikwaju ya penalti 5-4 katika mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi uliochezwa Januari 14, mwaka huu katika Uwanja wa Gombani, Pemba, visiwani Zanzibar, huku Yanga ikitaka kuendeleza heshima.
Azam na Yanga zitashuka dimbani katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 2:30 usiku.
Katika mchezo huo Azam inahitaji kulipa kisasi baada ya kupoteza mchezo wa mwisho huku Yanga ikisaka heshima na rekodi ya kuendelea kuwafunga ‘Wana Lambalamba’.
Akizungumza kuelekea katika mchezo huo, Kocha wa Yanga, Pedro Goncalves alisema wanakwenda kukutana na timu ngumu zaidi katika ligi, kwani Azam ina wachezaji wazuri.
Alisema kuwa walicheza nao katika fainali ya Kombe la Mapinduzi, hivyo anaamini wataingia na mbinu tofauti za kutaka matokeo, hivyo amejipanga vyema kuhakikisha anawakabili.
“Kucheza Uwanja wa Benjamin Mkapa ni fursa nzuri sana kwetu, uwanja una viwango vya kimataifa, hivyo ninaamini tutatumia vyema nafasi na kupata ushindi.
“Tunakwenda kukutana na moja ya timu bora Ligi Kuu Tanzania Bara, hivyo ninaamini mchezo utakuwa mgumu zaidi, lakini tutapambana kupata matokeo na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo.
“Tutaingia katika mchezo huo huku tukiwakosa baadhi ya wachezaji ambao ni majeruhi, hivyo lazima tuwe na mbinu mbadala kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema.
Nyota wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, alisema kwa upande wa wachezaji, wamejiandaa vizuri kuelekea katika mchezo huo ili kuweza kupata ushindi.
Alisema wanakwenda kukutana na wapinzani wagumu lakini wao wana morari ya kutosha kuhakikisha wanapambana mwanzo hadi mwisho ili kuweza kupata matokeo mazuri.
“Jukumu letu sisi wachezaji tutahakikisha hatuwezi kuruhusu bao lolote katika mchezo huo muhimu, tutapambana mwanzo hadi mwisho ili tuweze kupata ushindi na lengo letu kubwa ni kuhakikisha tunapata pointi tatu muhimu,” alisema Tshabalala.
Nyota huyo alisema kuwa wachezaji hawana hofu yeyote kuelekea katika mchezo huo, hivyo mashabiki na wapenzi wa timu yao wanatakiwa kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapa sapoti ya kutosha.
Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge alisema mchezo huo hautakuwa mwepesi kwani wanakwenda kucheza na nzuri na iliyotoka kupata matokeo mazuri katika mechi zake za hivi karibuni na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini watapambana kuwakabili.
Alisema kuwa wamefanya maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanapata ushindi japokuwa mchezo utakuwa na upinzani wa aina yake.
“Tunaingia katika mchezo huo tukijua utakuwa mgumu na wenye changamoto kubwa, kwani wapinzani wetu wapo kileleni mwa msimamo na wamekuwa na mwenendo mzuri wa matokeo, hivyo ninaamini tutawakabili na kupa ushindi,” alisema.
Kocha huyo alisema amesikitishwa na mchezo wao huo kuhamishiwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwani alihitaji wacheze katika Uwanja waliouzoea wa Azam Complex, lakini ana watafanya vizuri.
Kocha huyo alisema kuwa katika mchezo huo atawakosa baadhi ya wachezaji wakemuhimu ambao ni majeruhi, Edward Manyama, Yahya Zaid, Nassro Saduni na Abdul Suleiman ‘Sopu’.
Nahodha wa timu hiyo, Lusajo Mwaikenda alisema kuwa wamejipanga vizuri kwa asilimia 100 kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo.
Alisema wanategemea utakuwa mchezo mgumu kutokana na Yanga kuwa katika kiwango kizuri, lakini watafuata maelekezo ya benchi la ufundi kuhakikisha wanaibuka na ushindi.
“Sisi tutakaza buti kuwakabili Yanga, kwani tunahitahi kupata matokeo mazuri, tunajua mchezo utakuwa mgumu lakini hatutakubali kupoteza.
“Hatuna presha na mchezo baada ya kufanya maandalizi ya kutosha, tutafuata maelekezo ya benchi la ufundi kuhakikisha tunaibuka kidedea,” alisema.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga ipo kieleleni kwa pointi 35 katika mechi 13 ilizocheza huku Azam ikishika nafasi ya tatu kwa pointi 27 baada ya kucheza mechi 13.




