Na MWANDISHI WETU
UMAKINI mdogo umeiponza Yanga, baada ya kujikuta ikilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliofanyika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Yanga ambayo iliongoza kwa bao 1-0 tangu dakika ya 23, ililazimishwa sare kufuatia Ismail Mhesa wa Mtibwa kusawazisha bao hilo baada ya kupiga kona iliyojaa wavuni moja kwa moja.
Katika dakika za majeruhi, Yanga iliruhusu bao kutokana na umakini mdogo ambapo baada ya kupigwa kona, kipa Djigui Diarra aliamini Kouassi Yao ambaye alikuwa mbele yake angeokoa hatari hiyo lakini ilishindikana na mpira kujaa wavuni.
Mchezo ulianza kwa kasi huku timu zote zikishambuliana kwa zamu, kila moja ikitaka bao la mapema.
Dakika ya tisa, Yanga ilifanya shambulizi la kushtukiza ambapo Israel Mwenda alipata nafasi na kuingia na mpira ndani ya eneo la hatari lakini mabeki wa Mtibwa waliokoa hatari hiyo.
Yanga walifanya shambulizi jingine dakika ya 13 ambapo Allan Okello alipata nafasi, alishindwa kuitumia kwa wakati, mabeki wakaokoa hatari hiyo ikawa kona ambayo haikuzaa matunda.
Nyota wa Yanga, Pacome Zouzoua aliwainua katika viti mashabiki wa Yanga baada ya kufunga bao la kuongoza kwa shuti kali katika dakika ya 28.
Bao hilo, lilipatikana baada ya Okello kufumua shuti kali lililotemwa na kipa wa Mtibwa, Costantine Malimi kabla ya Emmanuel Mwanengo kuugonga na kumkuta Pacome akawuweka mpira wavuni.
Hata hivyo kipa Malimi alilazimika kutolewa nje dakika ya 28 baada ya kupata majeraha, nafasi yake ikachukuliwa na Toba Kutisha.
Mtibwa Sugar, nusura wasawazishe bao katika dakika ya 35 baada ya Said Mkopi kufumua shuti la mbali mpira ukagonga mwamba, mabeki wa Yanga wakaokoa.
Mchezo uliendelea kwa mshambulizi ya hapa na pale, hadi mapumziko ya kipindi cha kwanza, Yanga ilikuwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ya kushambuliana kwa zamu, dakika ya 47, Pacome alipiga faulo iliyotoka sentimeta chache nje ya lango.
Katika dakika ya 52, Mtibwa Sugar walijibu shambulizi, Mkopi alipata nafasi na kupiga shuti la mbali lililoishia mikononi mwa kipa wa Yanga, Diarra.
Dakika ya 61, Mwanengo nusura afunge bao baada ya kupiga mpira ambapo kipa wa Mtibwa, Kutisha aliudaka, Mwanengo mpira wa kurusha ulitoka kwa Kouassi Yao.
Yanga walifanya shambulizi jingine, dakika ya 78, Pacome alishindwa kuitumia nafasi baada ya kupaisha mpira juu akiwa ndani ya eneo la hatari, pasi ilitoka kwa Maxi Nzengeli.
Katika dakika ya 90, Mtibwa Sugar walisawazisha bao hilo kufuatia Mhesa kupiga mpira wa kona uliomshinda kudaka kipa wa Yanga, Diarra na kujaa wavuni moja kwa moja, hadi mchezo unamalizika, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
Kufuatia matokeo hayo, katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga imeendelea kubakia kileleni ikiwa na alama 38 baada ya kucheza mechi 16 huku Mtibwa ikifikisha pointi 22 katika mechi 17 ikipanda hadi nafasi ya saba.
Mtibwa iliwakilisha na Costantine Malimi/ Toba Kutisha, Oscar Masai, Haroun Lyawata, Datius Peter, Omar Selemani/ Juma Nyangi, Kassim Shaibu, George Chota/ Riphat Mrisho, Magata Charles, Andrea Simchimba/ Nassor Kiziwa, Said Mkopi/ Ismail Mhesa na Evance Fabian.
Yanga: Djigui Diarra, Frank Assink, Bakari Mwamnyeto, Maxi Nzengeli/ Aziz Andambwile, Mudathir Yahya/ Mohamed Damaro, Mohamed Hussein, Emmanuel Mwanengo, Pacome Zouzoua/ Buba Jammeh, Israel Mwenda/ Kouassi Yao, Duke Abuya na Allan Okello.




