Na REHEMA MAIGALA
BAADA ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuwataka Watanzania kulinda mali za umma na kueleza uwajibikaji si chaguo ila ni wajibu, wadau mbalimbali wakiwemo wasomi, wanasiasa na viongozi wa dini wamempongeza kwa kauli hiyo na kusema hakuna maendeleo pasipo na uwajibikaji mzuri.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na UHURU, wadau hao walisema uwajibakaji unaliletea taifa maendeleo na kuondoa changamoto zinazolikabili.
KATE KAMBA
Mwanasiasa mkongwe nchini Kate Kamba alisema, uwajibakaji katika shughuli mbalimbali unaleta usawa wa maendeleo.
Kamba alisema jamii na watumishi wa umma wafuate nyayo za Rais Dk. Samia anavyowajibika katika utendaji wake wa kazi bila ya ubaguzi wowote.
“Tunamuona Rais Dk.Samia anavyowajibika kwa Watanzinia bila ya kujali dini, kabila na jinsia,”alisema.
Kamba alisema mtumishi akifanya kazi zake inavyostahili hata maendeleo ya nchi yataonekana.
DK. RUGEIHYAM
Kwa upande wake mtaalamu wa Somo la Hisabati kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Silvester Rugeihyam, aliwaomba Watanzania waige nchi zilizoendelea.
Dk. Rugeihyam alisema kuna nchi nyingi zimeendelea kwa sababu ya kujituma kwa kuwajibika.
“Tunashuhudia nchi nyingi zimeendelea kwa sababu ya uwajibikaji mzuri katika shughuli zao za kujiongezea kipato,” alisisitiza.
Alisema uwajibikaji unaendana na uwajibishwaji hivyo, viongozi wa umma wajijengee tabia ya kuwajibisha watumishi wanaofanya ubadhirifu wa mali za umma.
“Hadi leo kuna baadhi ya watumishi wa umma wanatumia vibaya mamlaka yao ya kutumia mali za umma, hivyo wanatakiwa kuwajibishwa,”alishauri.
KIONGOZI WA DINI
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT, Sheikh Alhad Mussa Salum, alisema killa mtu katika eneo lake anatakiwa kuwajibika.
Alisema wafanyakazi wa umma wanatakiwa kuihudumia jamii kwa ufanisi mkubwa.
“Ukifanya hivyo ujue huo ndio uwajibikaji, hata mimi kiongozi wa dini ninatakiwa niwajibike kwa waumini wangu kuwapa mawaidha na kuwaamrisha kutenda yale yaliyo mema,”alisema.
Sheikh Alhad alisema kuwajibika ni ibada ,kwa sababu yoyote anayewajibika ipasavyo lengo lake kwake anataka kufanya yale yaliyo mema.
AGIZO LA RAIS
Juzi alipokea Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Rais Dk. Samia aliagiza uwajibikaji wa viongozi wa umma na Watanzania kulinda mali za umma.




