Na ZIANA BAKARI
BONDIA Nasra Msami, amewahimiza vijana kuwa mstari wa mbele katika kulinda amani kwa kuepuka kushawishiwa na mtu yeyote kuvuruga amani ya nchi.
Akizungumza na UHURU Dar es Salaam , bondia huyo alisema vijana wana nafasi kubwa ya kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na utulivu kupitia maamuzi sahihi na ushiriki wao katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Aliwasisitiza vijana kuwa ni muhimu kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa sheria na badala yake wajikite katika kazi halali zinazowajenga kiuchumi.
“Vijana wakifanya hivyo watasaidia kujenga taifa lenye mshikamano na maendeleo endelevu, hivyo niwaombe kuzingatia hili kwa umakini.
“Amani ni msingi wa mafanikio katika kila sekta, hivyo kila kijana ana wajibu wa kuilinda tunu ya taifa, bila amani, hata juhudi za maendeleo zinapotea,” alisema.
Pia, bondia huyo aliwasihi vijana kuwa mfano mzuri katika jamii kwa kuhubiri upendo, mshikamano na uvumilivu, ili kuimarisha umoja wa kitaifa.
Naye Patricia Nyamaka anayefahamika zaidi kwa mashabiki zake kwa jina la ‘Vene’ katika tamthilia ya ‘Kombolela’ msimu wa pili, amewasihi wasanii wenzake kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa amani nchini.
Msanii huyo amesema sanaa ina nguvu kubwa ya kufikisha ujumbe kwa watu wa rika zote.
“Nawaomba wasanii wenzangu, tuna wajibu wa kuelimisha jamii kuhusu amani, kupitia muziki, maigizo, filamu na sanaa nyingine,”alisema.
Aliongeza kuwa wasanii wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi.
“Wasanii tunapaswa kutumia majukwaa yetu kuhamasisha amani na kuepuka maudhui yanayoweza kuchochea migogoro au chuki katika jamii.
“Kila msanii ana kazi hiyo kwa nguvu zote, kwa mashabiki zake, amani ni msingi wa maendeleo ya sekta zote, ikiwemo sekta ya sanaa, hivyo wasanii wanapaswa kuilinda kwa nguvu zote,” alisema.
Alieleza kuwa bila amani, hata ubunifu na vipaji vya wasanii haviwezi kuonekana.




