Na NASRA KITANA
WAKATI kikosi cha Simba kikitarajiwa kushuka dimbani leo kupambana na Dodoma Jiji, kocha wa timu hiyo, Steve Barker amesema wamejipanga kupata ushindi.
Simba leo itawakaribisha Dodoma jiji katika mchezo wa wake wa 16 bora wa Kombe la Shirikisho(FA), utakaochezwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha saa 10:00 jioni.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Barker alisema pambano hilo litakuwa gumu kwa vile kila timu inahitaji kupata matokeo mazuri.
“Tumetoka kupata sare katika mechi iliyopita, tumefanyia kazi kasoro zote zilizojitokeza, hapa leng letu ni kupata ushindi.
“Pamoja na kushindwa kupata muda mzuri wa kufanya mazoezi lakini tumejitahidi kuondoa kasoro zote zilizokuwepo, tutapambana kwa nguvu zote kupata ushindi na kusonga hatua inayofuata,” amesema.
Barker alifafanua kuwa wamefanyia kazi kasoro zote zilizojitokeza katika mechi zilizopita.
Kocha huyo aliwaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuwapa sapoti timu ishinde mchezo wa leo.
Nyota wa timu hiyo, Rushine De Reuck alisema wachezaji wote wa timu hiyo, wana morari ya kutosha kuelekea pambano hilo.
“Tutaingia uwanjani kuhakikisha tunapambana kupata ushindi na kutumia vyema nafasi ambazo tutazipata, hatukuwa na matokeo mazuri hivyo hatutakubali kupoteza dhidi ya Dodoma Jiji,” alisema mlinzi huyo.
Naye kocha wa Dodoma Jiji, Aman Josiah alisema mechi dhidi ya Simba itakuwa ngumu lakini wao watahakikisha wanapata ushindi.
“Tumewaangalia wapinzani wetu vizuri na tumeona wapi kuna kasoro, hivyo tutahakikisha tunatumia udhaifu wa Simba kupata ushindi.
“Huu ni mchezo wa mtoano atakayefungwa anaondoka, nitakipanga vizuri kikosi changu kuhakikisha tunapata ushindi na kusonga mbele hatua inayofuata,” alisema kocha huyo.
Josiah alifafanua kuwa timu yake itaingia uwanjani katika pambano hilo, ikifahamu ni mchezo mgumu na wenye changamoto kubwa.
“Najua Simba hawajapata matokeo katika mechi mbili mfululizo hivyo watatumia mchezo huu ili kupata ushindi lakini sisi tumejipanga kupambana nao, kupata matokeo,” alisema Aman.
Mchezaji wa timu hiyo, William Edger alisema wachezaji wte wamejipanga vizuri kuelekea mchezo huo.
“Tunajua Simba ni timu bora hivyo tutaingia kwa kuwaheshimu na kucheza kwa nidhamu kubwa lengo ni kuhitaji ushindi na tutatumia kila mbinu ambazo mwalimu ametupatatia,” alisema William.
Nyota huyo amewaomba mashabiki na wapenzi wa timu yao kujaa kwa wingi uwanjani na kuwapa sapoti wafanye vizuri katika mchezo wa leo.




