Na SUPERIUS ERNEST
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amewataka vijana nchini, kushiriki katika shindano maalumu la kutafuta wazo bora bunifu la kiuchumi lenye lengo la kuimarisha ubunifu wa vijana na kupata mawazo chanya ya maendeleo endelevu ya Taifa.
Nanauka, alisema hayo jijini Dar es Salaam, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu shindano hilo na kutangaza kamati maalumu ya kuratibu shindano hilo.
“Baada ya kufanikiwa katika mashindano madogo, hivi sasa tumekuja na shindano kubwa la kupata wazo bora bunifu la kiuchumi, linalojulikana kama Vijana Uchumi Challenge.
“Vijana ndiyo nguvu kazi kubwa ya taifa ambayo ni asilimia 55.6.
“Ni nguvu kazi muhimu, tegemewa kwa taifa, wakitegemewa katika ubunifu mbalimbali wa kiuchumi na kidijitali katika kuchochea maendeleo, ndiyo maana tunakuja na shindano hili muhimu kwako,” alisema.
Alisema kupitia jukwaa hilo, wanawataka vijana kutoa wazo bunifu linalotekelezeka, likiendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo katika kulinda na kukuza maendeleo ya taifa dhidi ya changamoto za kiuchumi.
Alisema swali linalobeba shindano hilo, inapotokea changamoto ya kushuka kwa uchumi wa dunia, kwa sababu ya changamoto za kivita ni athari gani zitajitokeza na nini kifanyike kuepuka athari zinazoweza kujitokeza.
Nanauka, alisema lengo la shindano hilo, ni kupata mchango chanya kutoka kwa vijana katika kipindi cha sayansi na teknolojia kuwezesha kuchochea maendeleo ya taifa.
Alitaja zawadi ya washindi wa shindano hilo ni sh. milioni 50, huku akiwataka vijana kujitokeza kwani shindano hilo litafanyika pasipo na upendeleo.
Kwa mujibu wa waziri huyo, shindano hilo litaratibiwa na vijana wenyewe kupitia kamati maalumu aliyoiunda inayoundwa na vijana, ambapo wataandaa maandalizi ya awali, wataratibu na kuhakikisha washindi wanapatikana kwa uwazi pasipo upendeleo.
Waziri huyo, alisema kupitia Jukwaa la Vijana, wameanzisha mashindano madogo, ikiwemo ‘Idea Challenge’ kwa vyuo na vyuo vikuu na ‘idea kitaa’ maalumu kwa vijana wa mtaani.
Alisema kupitia jukwaa hilo, wamelenga na kupata mawazo ya vijana, kutimiza malengo na ubunifu wao kama inavyoeleza sera ya wizara ya vijana.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Joseph Malekela, alimshukuru waziri kwa kuwaamini katika kamati hiyo, huku akiahidi kutekeleza jukumu hilo kwa wakati na ushirikiano, ambapo leo wataanza rasmi.
Naye, Mjumbe wa kamati hiyo, Chrispina Kabale, alimshukuru waziri na viongozi kwa kuwaamini na watafanya kazi kwa ushirikiano kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.




