Na ATHNATH MKIRAMWENI
ONGEZEKO la abiria wanaotumia Reli ya Kisasa (SGR) kufikia milioni tano ndani ya muda mfupi, limewaibua baadhi ya wadau nchini wakiwemo wachumi.
Wakizungumza na UHURU, wachumi hao walisema mafanikio hayo ni mapinduzi ya kiuchumi yanayochochewa na usafiri wa uhakika, nafuu na haraka.
Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo alisema uwekezaji katika miundombinu ya reli ni hatua muhimu ya kufikia azma ya kuwa kitovu cha usafirishaji Afrika Mashariki na Kati.
Alisema uboreshaji wa reli hiyo, una mchango mkubwa katika kurahisisha usafiri wa watu na mizigo.
Akizungumzia ongezeko hilo la abiria, Profesa Kinyondo alisema hali hiyo inaonesha kuna mahitaji makubwa ya huduma ya usafiri wa reli.
Alieleza reli ni njia bora ya usafiri ikilinganishwa na barabara, maji na anga, kutokana na gharama nafuu na uwezo wake wa kusafirisha haraka.
Alisema usafiri wa reli unarahisisha wananchi kufikia masoko yenye bei nzuri zaidi ya bidhaa zao, akitolea mfano wakulima wa mazao ya mahindi, alizeti na zabibu.
“Hatua hii huongeza tija katika uzalishaji na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa, ninaishauri serikali kuongeza mabehewa ya kubeba abiria, mizigo na kuharakisha upanuzi wa reli kufikia mikoa mingine kama Mwanza na Kigoma,” alisema.
Alisema hatua hiyo itawezesha Tanzania kushindana na bandari zingine za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) Mohamed Maguo, alisema kasi ya usafiri wa SGR imekuwa kichocheo cha shughuli za kiuchumi na kijamii.
Pia imerahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa kwa muda mfupi, hivyo alishauri kuwepo takwimu za kabla na baada ya kuanzishwa usafiri huo ili kupima mchango wake katika kukuza uchumi.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa hirika la Reli Tanzania (TRC) Fred Mwanjala, alisema abiria milioni 5.5 walitumia usafiri huo kuanzia Juni, 2024.
Takwimu zilizotolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) zilionesha hadi Machi, mwaka huu, abiria 5,512,995 walisafiri kwa kutumia reli ya kisasa.
Alisema ongezeko hilo linaonesha SGR imejenga imani kubwa kwa watumiaji na kuwa chaguo kuu la usafiri ikilinganishwa na njia zingine.
“Mafanikio hayo yanaakisi ufanisi wa utoaji huduma, ambapo ratiba zimekuwa zikizingatiwa na uendeshaji kuwa wa kuaminika, hali inayodhihirisha uwezo wa TRC kusimamia miundombinu hiyo kwa ufanisi mkubwa.
Mwanjala alisema huduma ya SGR imeendelea kutoa mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii kwa kurahisisha usafiri kati ya Dar es Salaam, Morogoro na Dodoma.
Alisema mafanikio ya TRC yanaonesha uwekezaji wa serikali unaanza kuzaa matunda, ukichangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Tangu kuanza safari za treni ya SGR hadi kufikia Machi mwaka jana, TRC iIisafirisha abiria 2,054,828 na kuwezesha kukusanya mapato ya sh. bilioni 60.2.



