Na MWANDISHI WETU
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Dk. Seif Shekalaghe, ameeleza mkakati wa miaka mitatu utakaoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika nafasi yake ya Bingwa wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, unaolenga kusaidia nchi za Afrika kupunguza na kutokomeza vifo vya wajawazito vinavyozuilika.
Dk. Shekalaghe, alisema hayo jijini Dar es Salaam, juzi, katika Kikao cha Kamati ya Kitaalamu (TWG 5) ya Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto.
Alisema Tanzania imeandaa andiko la dhana litakalotumika kama mwongozo wa kushirikisha mataifa mengine ya Afrika kujifunza kutokana na mafanikio ambayo imeyapata licha ya kuwa na rasilimali chache.
“Baada ya kufanya tathmini ya mazingira ya kila nchi, tutaandaa viashiria muhimu vya kufuatilia maendeleo na afua mahsusi
zitakazotekelezwa.
Mfumo wa ufuatiliaji na tathmini, utawekwa kuhakikisha hatua zinazochukuliwa, zinaleta matokeo yaliyokusudiwa,”alisema.
Alisema lengo kuu la mpango huo ni kuhakikisha ifikapo mwisho wa
kipindi cha miaka mitatu cha ubingwa wa Rais Samia, nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, zitapiga hatua kuboresha afya ya uzazi na kupunguza vifo vya kinamama na watoto vinavyozuilika.
“Tunaamini lengo hili, linawezekana kufikiwa ikiwa nchi zitaendelea kushirikiana, kujifunza kutoka kwa uzoefu wa wenzao na kuwekeza katika afua zenye tija kwa afya ya mama na mtoto,” alisema.
MKURUGENZI IDARA YA AFYA
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk. Ahmad Makuwani, alisema mafanikio ambayo Tanzania imepata katika kuboresha afya ya uzazi, mama na mtoto, ndiyo msingi unaoiwezesha nchi kushiriki kikamilifu katika jitihada za kikanda za kuboresha afya ya uzazi barani Afrika.
Dk.Makuwani alisema tangu Rais Dk. Samia aanze kuongoza nchi, serikali imeendelea kuwekeza katika afua za afya ya uzazi, mama.




