Na MUSSA YUSUPH,
Dodoma
WABUNGE wameendelea kuibana serikali kuhusu pendekezo la kuongeza kodi ya usajili wa pikipiki maarufu bodaboda kutoka sh. 95,000 hadi sh. 150,000, wameshauri pendekezo hilo ni vyema likaondolewa.
Wamesema pendekezo hilo huenda likakwamisha vijana kutumia usafiri huo kama sehemu ya kujiingizia kipato kupitia biashara ya usafirishaji abiria.
Hayo yalibainishwa bungeni, jijini Dodoma na baadhi ya wabunge walipochangia mjadala kuhusu Hali ya Uchumi wa Taifa kwa mwaka 2025, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2025/26, Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2025/26 na Mapendekezo ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2026/27.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Clayton Chipando maarufu Baba Levo, aliishauri serikali kuondoa ongezeko la kodi ya bodaboda na kuihamishia katika pombe.
Alieleza kuwa, haungi mkono hoja ya kuongeza sh. 45,000 katika kodi za bodaboda, kwani haitasaidia vijana kujikwamua kiuchumi.
Chipando, alisema yeye ni miongoni mwa vijana ambao hawajapata elimu ya juu, hivyo yupo tayari kuwatetea vijana hao wasibebeshwe mzigo wa tozo ambazo zitarudisha nyuma maendeleo yao.
TASKA MBOGO
Mbunge Viti Maalumu Mkoa wa Katavi, Taska Mbogo, aliishauri serikali kufanya mapitio ya kodi zinazotozwa kwa waendesha bodaboda.
Alisisitiza kuwa, ongezeko la kodi hiyo, inaweza kuwakwaza vijana kiuchumi badala ya kuwasaidia.
“Bodaboda ni sekta muhimu inayowapatia kipato vijana wengi nchini, hivyo inahitaji mazingira rafiki ya kifedha ikue na kuchangia maendeleo ya taifa.
Ongezeko la kodi linaweza kuleta changamoto kwa waendesha bodaboda,” alisisitiza.
Aliishauri serikali kuangalia upya mfumo huo kuhakikisha unalinda na kuimarisha uchumi wa vijana wanaojishughulisha na shughuli hiyo.
RAHMA RIYADH KISUO
Mbunge wa Viti Maalumu, Rahma Riyadh Kisuo, alisema ongezeko la kodi katika sekta ya michezo ya kubahatisha, itaathiri shughuli za biashara na kupotea ajira nchini.
Aliishauri serikali inapaswa kuangalia kwa makini athari za ongezeko hilo kabla ya kulitekeleza.
Alisisitiza kuwa, iwapo kodi ya asilimia tano itaongezwa, ni vyema ikaelekezwa kwanza katika michezo ya kubahatisha inayofanyika mtandaoni kuliko waendeshaji wa vituo vya michezo ya kubahatisha.
“Nashauri ongezeko la kodi la asilimia tano lianze moja kwa moja katika ‘internet betting’ kwanza.
“Likipelekwa katika ‘retail-based casinos’ tunakwenda kuua kabisa operesheni za biashara hizo,”alisisitiza.
Alibainisha kuwa, sekta hiyo kwa sasa inatoa ajira 2,000 za moja kwa moja na zaidi ya ajira 4,000 zisizo za moja kwa moja, hivyo ongezeko la kodi linaweza kuathiri uwezo wa waendeshaji kuendelea na shughuli zao.
“Tunapokwenda kuongeza kodi, tunakwenda kuua operesheni na tunapoua operesheni tunakwenda kuua ajira zaidi ya 4,000,” alisema.
NJALU AGUSIA UKUSANYAJI MAPATO
Mbunge wa Itilima (CCM), Njalu Silanga, alisema serikali inaweza kugharimia bajeti yake kupitia mapato ya ndani endapo itaboresha mikakati ya ukusanyaji na kutumia kwa ufanisi rasilimali zilizopo, ikiwemo nguvu kazi, madini, mito na vyanzo vingine vya uchumi.
Mbunge huyo, alimshauri Waziri wa Fedha, Balozi Khamisi Mussa Omar, kufuatilia kwa makini kampuni inayohusika na uwekaji stempu katika viwanda vya vinywaji, akidai inapata zaidi ya sh. bilioni 400 wakati serikali haipati faida ya kutosha.
Njalu alisisitiza kuwa, kazi hiyo ingefanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato.
ANNE KILANGO
Mbunge wa Same Mashariki (CCM) Anne Kilango, aliwataka wazazi na walezi kujikita zaidi katika malezi ya watoto, kujenga taifa lenye maadili na nidhamu bora.
Alisema kuna mwelekeo wa wazazi kuachia malezi kwa wafanyakazi na waendesha bodaboda, hali inayochangia mmomonyoko wa maadili kwa watoto.
Anne alisema ni muhimu wazazi kurejea katika nafasi yao ya msingi ya malezi, kuwalea watoto katika maadili mema yatakayosaidia kujenga mustakabali bora wa taifa.




