Na WILLIUM PAUL, Kilimanjaro
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, kesho anatarajia kuzindua jengo la tiba mionzi katika Hospitali ya Rufani ya Kanda KCMC mkoani Kilimanjaro, lenye thamani ya sh. bilioni 17.
Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa Rais Dk. Samia mkoani humo.
Alisema Rais Dk. Samia, anatarajia kuwasili mkoani humo kesho kwa ziara ya siku moja.
Alisema lengo la ziara hiyo ni kuzindua jengo la tiba ya mionzi katika Hospitali KCMC, ambalo limegharimu sh. bilioni 17, likiwa na vifaa vyake.
Kwa mujibu wa Babu, kati ya fedha hizo, serikali imechangia kiasi cha shilingi bilioni 5.5.
Babu alisema uchangiaji huo wa serikali ni mwendelezo wa kushirikiana na wadau pamoja na taasisi zisizo za serikali kuwaletea wananchi maendeleo.
Babu alisema kila mwezi, imekuwa ikitoa sh. bilioni moja kulipa mishahara ya watumishi katika hospitali hiyo.
“Rais Dk. Samia atafanya ziara ya kikazi ya siku moja Kilimanjaro, lengo la ziara yake ni kuja kufanya kazi ya uzinduzi wa jengo la tiba mionzi katika Hospitali ya KCMC.
“Mkumbuke kuwa, jengo hili liliwekwa jiwe la msingi na yeye mwenyewe Oktoba 16 mwaka 2021, hivi sasa limekamilika,”alisema.




