Na MWANDISHI MAALUMU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuvutia uwekezaji wenye tija, unaochochea ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda, uhamishaji wa teknolojia na ajira kwa Watanzania.
Aidha, amesema serikali imepokea nia ya Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Dangote Group, Alhaj Aliko Dangote, ya utayari wa kampuni yake, kupanua ushirikiano wa uwekezaji katika sekta mbalimbali za kimkakati.
Rais Dk. Samia, alisema hayo Ikulu, jijini Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Dangote Group, Dangote.
Kutokana na nia hiyo ya Dangote, Rais Samia, alizielekeza wizara na taasisi husika, kuendelea na majadiliano ya kitaalamu kuhusu maeneo yaliyojadiliwa, kwa kuzingatia sera, sheria na vipaumbele vya maendeleo ya nchi.
Dangote, ambaye ni mwekezaji na mfanyabiashara kinara barani Afrika, alieleza utayari wa kampuni yake kupanua ushirikiano wa uwekezaji na serikali katika sekta mbalimbali za kimkakati.
Mazungumzo hayo, yaligusa maeneo ya miundombinu ya usafirishaji, uzalishaji wa mbolea nchini na nishati, ikiwa ni sehemu ya fursa za uwekezaji zinazochochea shughuli za kiuchumi nchini na katika ukanda.
Dangote alisema Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji na fursa kubwa za kukuza viwanda vinavyoongeza thamani ya malighafi na kuchochea biashara ya kikanda.
“Tumetambua maeneo yenye manufaa makubwa kwa Tanzania na tuko tayari kushirikiana na Serikali kuyaendeleza kwa manufaa ya pande zote,” alisema.
WALIPOKUTANA MEI 16, 2026
Mei 16, mwaka huu, Rais Dk. Samia, alikutana na kuzungumza na Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Dangote Group, Alhaji Dangote, Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Katika mazungumzo yao, walijadili kuhusu kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na kampuni za Dangote katika nishati, viwanda, bandari, gesi, mbolea na miundombinu.
Rais Samia alimhakikishia ushirikiano na kumwomba Alhaji Dangote, aendelee kuangalia fursa zaidi za biashara na uwekezaji nchini zenye tija na manufaa kwa mwekezaji, serikali na taifa kwa ujumla.
Aidha, Rais Samia, aliikaribisha Dangote Group, kuwekeza katika uzalishaji wa mbolea nchini, akibainisha kuwa, mahitaji ya bidhaa hiyo ni makubwa kuliko uwezo wa sasa wa uzalishaji wa ndani.
Katika mjadala huo, Alhaji Dangote, alitumia fursa hiyo kuipongeza serikali kwa kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji na kutatua changamoto za wawekezaji nchini.
Pia, alielezaa hatua za serikali kutatua changamoto zilizokuwa zikikabili shughuli za Kiwanda cha Saruji cha Dangote, mkoani Mtwara, zimeongeza tija na ufanisi wa uendeshaji na imani ya kampuni hiyo kwa Tanzania kama eneo muhimu na la kimkakati la uwekezaji barani Afrika.




