Na EMMANUEL MOHAMED
MAMLAKA ya Mapato ya Tanzania (TRA), imesema makusanyo ya kodi yamefikia sh. trilioni tatu kwa mwezi.
Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, alisema hayo, alipokuwa akitaja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 30 tangu kuanzishwa mamlaka hiyo.
Mwenda alitoa kauli hiyo katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari, kuelekea Siku ya Tuzo ya Rais kwa Mlipakodi Bora na Maadhimisho ya Miaka 30 ya TRA jijini, Dar es Salaam.
“Kabla ya Julai Mosi mwaka 1996 kodi nchini ilikuwa inasimamiwa na Wizara ya Fedha, ambapo tulikuwa na idara tatu ambazo zilikuwa zinafanya kazi pekee yake, Idara ya Forodha, Idara ya Kodi ya Mauzo na Kodi ya Mapato
“Kipindi cha awamu ya pili cha Rais Mzee Ali Hassan Mwinyi, kulikuwa na Tume ya Mzee Mtei, wakaunda kuona namna gani nchi ijitegemee na moja ya mapendekezo yalikuwa kuwa na chombo kimoja ambacho kinasimamia masuala ya kodi nchini,”alisema.
Alisema Mwinyi aliteua Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ambapo Sheria ilipitishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1995 na ilipofika Julai Mosi mwaka 1996 TRA ilianza kazi rasmi.
“Ilipoanza tu yale ambayo yaliyosababisha kuundwa kwake, yalianza kufanyiwa kazi, kwanza kabla ya TRA kuanza mwaka 1995, makusanyo ya kodi kwa mwezi kwa nchi nzima kwa idara zote tatu ilikuwa sh. bilioni 24.3
“Lakini, ilipoanza mwaka 1996, ilifanya kazi katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia Julai 1996 hadi Juni 1997 makusanyo yaliongozeka na kufikia sh. bilioni 44.3 kwa mwezi
“Sasa leo tumetimiza miaka 30 ambapo kabla ya TRA, tulikuwa tunakusanya sh. bilioni 24.3 kwa mwezi, kwa mwaka ilikuwa sh. bilioni 292 leo tutakapomaliza mwezi Juni tutakuwa tunakusanya sh. trilioni tatu kwa mwezi,” alisema.
Kamishna huyo, alisema kutoka sh. bilioni 24.3 kwa mwezi hadi sh. trilioni tatu ni mafanikio makubwa ambayo yamefanyika nchini kwa walipakodi wote na kuifanya Tanzania iwe na maendeleo, ijitegemee.
“Kuna kila sababu, ikifika siku hiyo kuwashukuru walipakodi na Watanzania wote kwa namna ambavyo wanajitoa kulipa kodi kwa hiyari na kupandisha mapato yalipotoka hadi hapa,”alisema.
Aidha, alisema wakati TRA inaanzishwa, kulikuwa na walipa kodi 7,500 ambapo hadi hivi sasa kuna walipa kodi milioni 8.4 wakiwemo wawekezaji, waajiriwa na wafanyabiashara.
“Bado kuna kazi kubwa ya kufanya ya kuongeza idadi hiyo, nchi yetu ina idadi ya watu milioni 60, lakini siyo wote wanastahili kulipa kodi tukitoa watoto, wazee kuna kama milioni 34 ya watu ambao wanatakiwa kulipa kodi
“Katika watu milioni 8.4 kati ya watu milioni 34 wanaostahili kulipa kodi bado idadi ya walipa kodi ni ndogo, sasa tunaposherehekea miaka 30 lazima tujiulize tunafanya nini ili kuongeza idadi hiyo ya walipa kodi
“Tuna kila sababu ya kujipongeza tumetoka mbali tunakwenda kwa hatua na tutafika kule tunapotaka kufika, tunaposherehekea miaka 30 mahusiano na walipa kodi na TRA ni mazuri na ya karibu,”alisema.
Mwenda alidokeza kuwa, wakati TRA inasema imefikia makusanyo ya sh. trilioni tatu kwa mwezi, Tanzania inazidi kuendelea, hivyo inahitaji fedha zaidi makusanyo yaendelee kupanda.
“Kazi yetu ni kuwezesha biashara hatutakubali TRA kuona biashara inakufa kwa vitu ambavyo tuna uwezo wa kusaidia, na moja ya vitu ambavyo tunasaidia ni hata kuruhusu kodi kulipwa kwa awamu na uwezeshaji huo umeongezeka sana
“Tunaona misamaha mingi sana imetolewa, tumeona marejesho ya kodi yanalipwa sana kwa watu wenye madai mwaka jana, mwaka juzi tumelipa zaidi ya sh. trilioni 1.2, ni marejesho kwa ajili ya kuwawezesha mtaji wa uendeshaji wa biashara ili ziendelee,”alisema.
Alisema hiyo ni moja ya njia ya kuwezesha biashara ambayo imefanywa katika kipindi cha miaka 30 na TRA imejitahidi kuleta usawa wa ulipaji kodi kwa wote.
“Huduma za TRA zimeongezeka, wakati tunaanza tulikuwa hatuna hata ofisi wilayani, leo tuna ofisi kila wilaya wigo wetu ni mkubwa wa utoaji wa huduma
“Kuna uwekezaji mkubwa ambao Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameufanya. Katika ofisi zetu kuna vifaa vya kisasa, magari ambayo yanatembea kama ofisi, maofisa ambao wamepata mafunzo kwa weledi kwa ajili ya kuwezesha biashara za Watanzania kwenda vizuri,”alisema.
Alisema wakati TRA ilipokua inaanza uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa (GDP) ilikuwa chini ya asilimia nane, lakini hivi sasa imefikia asilimia 14 hatua inayoonesha makusanyo ya kodi yameongezeka.
TUZO YA RAIS DK. SAMIA
Katika hatua nyingine, Kamishna huyo, alisema Julai Mosi, Rais Dk. Samia, anatarajia kuwakabidhi tuzo ya Rais kwa mlipa kodi bora, katika hafla itakayofanyika Mlimani City jijini Dar es Saalam.
Mwenda alisema kitendo hicho cha Rais Dk. Samia kuwakabidhi tuzo walipa kodi wanaotokea mikoa 33 ya kikodi tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1962 haijawahi kutokea.



