Na MUSSA YUSUPH, Dodoma
SERIKALI imesisitiza kwamba usalama, amani na utulivu ni kipaumbele namba moja kisichokuwa na mjadala huku ikionya haitovumilia vitendo vya uvunjifu wa sheria, uchochezi na fujo za aina yoyote.
Pia, imeonya hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi dhidi ya watu au kikundi chochote kitakachobainika kutaka kuharibu amani na utulivu nchini.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu, Dk. Mwigulu Nchemba katika hotuba yake ya kuhairisha Mkutano wa Tatu wa Bunge la 13, bungeni jijini hapa.
Alisema serikali iko imara kuendelea kutimiza kikamilifu wajibu wa kulinda mipaka ya nchi, usalama wa raia, mali, umoja, amani, mshikamano na muungano.
“Ninawasihi Watanzania wote kuheshimu misingi ya utawala bora na kuhakikisha shughuli mbalimbali za kijamii, kiutamaduni, kidemokrasia na kisiasa zinaendelea kufanyika kwa kuzingatia sheria, taratibu, mila, desturi na katiba ya nchi yetu,”alifafanua.
Alisisitiza: “Serikali iko imara na itaendelea kutimiza kikamilifu wajibu wa kulinda mipaka ya nchi yetu, usalama wa raia, mali na tunu za taifa ikiwemo umoja, amani, mshikamano na muungano.”
UMUHIMU WA AMANI
Waziri Mkuu alisema uwepo wa amani umeendelea kuwa msingi muhimu wa shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo kuifanya nchi kuendelea kuvutia uwekezaji na kuimarisha ustawi wa wananchi.
Alibainisha kuwa, Watanzania wana wajibu kutunza hali hiyo bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kikabila.
“Nitoe rai kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa analinda na kuitunza tunu ya amani na utulivu wa nchi yetu. Nawasisitiza Watanzania wenzangu tuendelee kulinda amani tuliyoirithi kwa wazee wetu kwa kuzingatia sheria, kuheshimu haki za wengine na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kusababisha migawanyiko.
Waziri Mkuu aliongeza: “Tuzingatie matumizi ya lugha ya staha katika mijadala ya kijamii na kisiasa, kwani yana mchango mkubwa katika kuvunja mshikamano wa kitaifa. Amani ikivunjika, hakuna anayejihakikishia usalama, hasa hasa wale wanaoishi nje ya Tanzania waituongoze kuvunja amani ya nchi yetu. Tusidanganyane amani, ulinzi na usalama sio suala la kujadiliwa.”
DEMOKRASIA
Dk. Mwigulu alisema Tanzania imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki katika masuala ya kisiasa kwa njia ya amani na ustaarabu.
Alibainisha kuwa, demokrasia inatoa nafasi kwa watu kutoa maoni yao, kuchagua viongozi na kushiriki katika maendeleo ya taifa kwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa.
“Sina shaka mtakubaliana nami kuwa kuendesha siasa za kistaarabu ni msingi wa kuimarisha amani na demokrasia. Viongozi wa vyama vya siasa, wafuasi wao pamoja na wananchi kwa ujumla wanapaswa kujenga utamaduni wa kuheshimu tofauti za mawazo, kuepuka lugha za uchochezi na kuweka mbele maslahi ya taifa letu.
“Unapotaja suala la uendelezaji wa demokrasia nchini Tanzania, huwezi kuliongelea jambo hili bila kugusia jitihada binafsi za Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Wakati wote amekuwa kinara katika kuimarisha demokrasia, haki za binadamu na utawala bora,” alieleza.
Alisema katika kipindi chote cha uongozi wa Rais Dk. Samka nchi imeshuhudia utekelezaji falsafa yake ya 4R yaani maridhiano, ustahimilivu, mageuzi na mabadiliko ambayo yamekuwa chachu ya kuimarisha siasa za ndani ya nchi.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kutokana na utashi wa Dk. Samia, nchi imeendelea kuwa na mshikamano, amani na umoja wa kitaifa.
“Hii ni kutokana na msisitizo wake kuhusu utekelezaji wa masuala ya haki za binadamu, utawala bora na demokrasia. Isitoshe, tumeshuhudia maboresho mbalimbali ya upande wa mifumo, sheria na uendeshaji wa shughuli za kisiasa,” alifafanua.
Vilevile, alisema Watanzania wameshuhudia uwepo wa fursa zaidi za mijadala na maridhiano miongoni mwa makundi ya wadau wa demokrasia na masuala ya siasa.
“Ni lazima tukubali kuwa kupitia kuimarisha maridhiano baada ya uchaguzi, kuendeleza demokrasia na kuendesha siasa za kistaarabu, taifa linaweza kuendelea na kustawi kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo.
“Ninaendelea kuamini kwamba bila kujali tofauti zetu za kifikra, kiitikadi na imani zetu na hata kama tukifarakana na kutofautiana kiasi gani, namna pekee ya kuonesha uzalendo na mapenzi mema kwa nchi yetu ni pale tunapokubali kuwa tayari kukaa kwenye meza ya mapatano na huo ndiyo uongozi, uzalendo na ukomavu wa kisiasa,” alisisitiza.
Alisisitiza: “Tunapaswa kuijali nchi yetu kwanza kwa kukaa kwenye meza ya maridhiano na kutanguliza utaifa wetu kwanza.”
MSHIKAMANO WA KITAIFA
Kwa mujibu wa Dk. Mwigulu, amani, utulivu na mshikamano wa taifa siyo vitu vya kuchezewa kwani vimejengwa kwa jasho, uzalendo, damu na hekima za waasisi.
Alieleza kwa namna yoyote ile serikali haitaruhusu viharibiwe kwa tamaa za kisiasa au maslahi ya wachache.
“Tanzania ni nchi yetu sote na hatutakuwa tayari kuona mtu yeyote, kikundi chochote au maslahi yoyote yakilitumbukiza taifa letu katika mgawanyiko, vurugu au machafuko.
“Umoja wa Watanzania si jambo la mjadala; ni msingi wa uwepo wa taifa letu na ni wajibu wa kila mmoja kuutunza. Hivyo, tuipende, tuilinde na kuipigania nchi yetu na tusikubali kugawanyika kwa misingi ya rangi, ukabila, dini au ukanda ili tuendelee kuwa na amani na kufikia kiwango cha juu cha ustawi na maendeleo.
Aliongeza: “Suala la usalama, amani na utulivu ni kipaumbele namba moja na hakuna mjadala katika hilo. Niwahakikishie waheshimiwa wabunge na wananchi kwa ujumla, vitendo vya uvunjifu wa amani, uchochezi na fujo za aina yoyote havitavumiliwa na mamlaka husika. Hatua stahiki zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria za nchi.”
UCHAGUZI
Katika usimamizi wa shughuli kwenye mamlaka za serikali za mitaa, alisema kila mwaka serikali inaingia gharama za uchaguzi wa naibu meya na makamu wenyeviti wa halmashauri.
Alisema mazingira hayo yanazorotesha utendaji, yanachochea migongano na kuondoa utulivu kwenye mamlaka za serikali za mitaa.
Waziri Mkuu alibainisha kuwa, katika mkutano ujao wa Bunge, serikali itawasilisha mapendekezo ya marekebisho ya sheria kuhusu nafasi za Naibu Meya na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri.
“Tuaondoa uchaguzi kufanyika kila mwaka. Lengo ni kubadilisha mfumo wa sasa na kuwa na Naibu Meya na Makamu Mwenyekiti kuwa kiongozi kwa kipindi chote cha uhai wa Baraza la Madiwani.
“Marekebisho hayo yanatarajia kuleta utulivu, viongozi wajikite katika kufanya kazi na kujiekeleza kwenye shughuli za maendeleo ya wananchi katika maeneo yao. Mambo ya safu na kuwaza uongozi ni ubinafsi,” alifafanua.
ATOA ONYO KALI
Katika hatua nyingine, Dk. Mwigulu alisema kumejitokeza vitendo vya baadhi ya watendaji wa mamlaka za udhibiti na usimamizi wa sheria kunyang’anya bidhaa, mitaji na vitendea kazi vya wajasiriamali mbalimbali.
Alisema vitendo hivyo havikubaliki, kwani vinarudisha nyuma jitihada za wananchi kujikwamua kiuchumi, licha ya serikali kuweka mazingira mazuri ya kuwawezesha wananchi waweze kutekeleza majukumu yao.
“Kama msimamizi wa shughuli za kiserikali nitaendelea kuchukua hatua kali ili kukomesha tabia hii.
“Niendelee kusisitiza maelekezo ya serikali kwa watendaji kuheshimu jasho la mtanzania, shughuli zainazofanywa na mtanzania, mitaji na shughuli zinazofanywa na wajasiriamali kote nchini,”alisisitiza.
Alionya: “Dosari zozote zinazojitokeza katika shughuli zao zishughulikiwe kwa kutumia njia zisizohusisha kukamata mali na mitaji yao isipokuwa kwa makosa ya kijinai na yanayohatarisha usalama.”



