ATHNATH MKIRAMWENI na LILIAN JOEL, Arusha
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Edwin Mtei (94), anamkumbuka kama miongoni mwa watumishi na viongozi wenye mchango mkubwa katika ujenzi wa taifa hususan eneo la fedha, mipango na uchumi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kutiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari Machumu, ilisema Mtei alifariki dunia juzi,usiku, jijini Arusha.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa niaba yangu binafsi, natuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo,” alisema Rais katika taarifa hiyo.
Alisema Mzee Mtei alihudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo ya Gavana waKwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuanzia mwaka 1966 hadi 1974 na kushiriki kuimarisha misingi ya uendeshaji wa benki hiyo na uthabiti wa mfumo wa fedha nchini.
Rais Samia, alisema Mzee Mtei ataenziwa katika historia ya siasa za vyama vingi kama miongoni mwa waasisi wa demokrasia ya ushindani wa vyama, akitajwa kuwa ni miongoni mwa waanzishi wa Chama cha Demokrasia ya Maendeleo (CHADEMA).
Kwa mujibu wa Rais Dk. Samia, mchango wa Mzee Mtei, utaendelea kukumbukwa na kuenziwa na vizazi vya sasa na vijavyo hususan, kupitia maandiko yake binafsi yanayoeleza safari yake ya maisha na utumishi wake wa uongozi katika kuijenga Tanzania.
Aidha, Rais Dk.Samia aliwaombea faraja, nguvu na amani, familia, ndugu na wafiwa wote na kumwomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.
GAVANA EMMENUEL TUTUBA ATOA NENO
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania(BoT), Emmanuel Tutuba, alisema benki hiyo, itamkumbuka Mzee Mtei kwa utumishi wake uliotukuka.
“Hakika, Mzee Mtei atakumbukwakwa utumishi wake uliotukuka, uliomwezesha kushika nafasi za uongozi muhimu kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Gavana wa Kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania na baadaye Waziri wa Fedha wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Kwa niaba ya Bodi, Menejimenti na watumishi wa BoT, tunatoa pole kwa wanafamilia wote, ndugu, jamaa, marafiki na majirani wa mzee Mtei kutokana na msiba huo mkubwa.
“Tunamwomba Mwenyezi Mungu awape ustahimilivu na faraja ya kweli, watu wote walioguswa na msiba huu,” alisema.
CHADEMA WAOMBOLEZA
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, alisema wamepoteza nguzo imara.
“Tunachukua nafasi hii, kutoa pole kwa familia ya Mzee Mtei, ndugu, jamaa na marafiki, CHADEMA imepoteza moja ya nguzo imara za chama chetu.
“Tutamwenzi Mzee Mtei kwa mema aliyoyafanya kwa chama na nchi yetu.Pumzika kwa amani Mzee Mtei,”alisema.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa wa Mawasiliano na Uenezi wa Chadema, Brenda Rupia, ilieleza kuwa, chama hicho kimetangaza siku saba za maombolezo kuanzia jana.
Brenda, alisema Mtei alifariki dunia siku moja kabla ya Chadema hakijaadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwake, Januari 21, 1993 ambapo alikabidhiwa cheti cha usajili wa chama hicho.
WASOMI WAMWELEZEA
Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dk. Philip Daninga, alisema Tanzania imempoteza mtu mwenye mchango katika sekta ya uchumi na maendeleo ya nchi.
“Tumepoteza nuru ya Tanzania, tunayohitaji kwa ushauri na busara. Mzee Mtei alikuwa na mchango chanya na kuisaidia BoT na uchumi kwa ujumla, ninaweza kusema ni miongoni mwa wasomi ambao nchi inajivunia kwa nafasi zao,” alisema.
Aliwashauri Watanzania kujifunza mema aliyoyaacha, kwani alikuwa mchapakazi na mtu mwenye weledi kwa sekta ya uchumi.
DK. RICHARD MBUNDA
Mchambuzi wa Masuala ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM), Dk. Richard Mbunda, alisema Mzee Mtei ni kiongozi na nguzo muhimu ya kuendesha uchumi.
“Mzee Mtei anatufundisha uhusiano uliopo karibu, kati ya siasa na uchumi, aliamininchi ipige hatua tunahitaji tuendane na sera za soko huru, hivyo ni mtu aliyetoa mchango kujaribu kuboresha sera zetu kisiasa na jinsi zinavyoratibu sera za uchumi,” alisema.
Aliwaasa viongozi wanapostaafu kutokukaa kimya, waangalie namna ya kutoa mchango chanya kwa jamii kutokana na uzoefu wao serikalini kwa lengo la kuliletea Taifa maendeleo.
MTOTO WA MTEI AZUNGUMZA
Mtoto wa Mzee Mtei, Nelly alisema baba yake alifariki usiku wa Januari 19, mwaka huu.
“Tunatarajia kumzika babaJumamosi shambani kwake Tengeru,Wilaya ya Arumeru,mkoani Arusha Januari 24, mwaka huu,”alisema.
Alisema familia itamkumbuka kwa moyo wake wa upendo, ucheshi wake na uwezo wa kuishi na watu wa rika zote.
“Kwa kweli, Baba alikuwa na upendo hasa kwa familia yake tutamkubuka kwa hilo, alikuwa anapenda watu wasome, alithaminielimu,” alisema.
Alisema baada ya baba yake kustaafu utumishi wa umma, alijikita katika shughuli za kilimo na alipenda kulima kahawa.
“Hili shamba la kahawa mnaloliona hapa nyumbani, alinunua mwaka 1980 na akahamia hapa, akajenga makazi yake hadi umauti ulipomfika,”alisema.
Mzee Mtei alizaliwa Julai 12, 1932, Marangu mkoani Kilimanjaro,ameacha watoto watano.




