Na NASRA KITANA
WAKATI droo ya michuano ya ‘Kagame Cup’, ikitarajiwa kufanyika leo, timu za Simba na Singida Black Stars zipo mbioni kutua nchini Rwanda.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kufanyika Julai 24 hadi Agosti 7, mwaka huu nchini Rwanda,
Jumla ya timu 12 zinatarajiwa kushiriki mashindano ya mwaka huu ambazo ni bingwa mtetezi Singida Black Stars, Simba kutoka Tanzania na KVZ ya Zanzibar.
Zingine ni APR na Rayon Sports za Rwanda, Vipers (Uganda), Al Hilal na El Merriekh (Sudan), Gor Mahia (Kenya), Mogadishu City (Somalia), Jamus (Sudan Kusini) na FC Garde Républicaine ya Djibouti.
Droo hiyo, itafanyika leo katika nchini Rwanda kuanzia saa 4:00 asubuhi, ikiwa ni maandalizi ya mashindano hayo yatakayochezwa katika viwanja vya Kigali Pele na Amahoro.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mratibu wa klabu ya Simba, Abbasi Ally alisema kuwa timu yao inatarajiwa kutua nchini Rwanda, Julai 21, mwaka huu.
“Angalia Ligi Kuu Tanzania Bara itaanza mwezi Agosti mwanzoni, tutashiriki mashindano hayo, kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu.
“Tumefikiria kwa kina na kuamua kwenda kushiriki mashindano hayo awali tuliona kama ratiba inabana, tunataka kufanya maandalizi yetu ya msimu ujao , tutakuwa na muda mzuri wa maandalizi,” alisema Abasi.
Kwa upande wa Ofisa Habari wa Singida BS, Hussein Massanza alisema timu yao imethibitisha ushiriki katika mashindano hayo, lakini imeweka kipengele cha kulipwa fedha zao za ubingwa wa msimu uliopita ndio washiriki.
Awali, Singida BS walikuwa wakidaiwa kuwa huenda wasishiriki kutokana na kutopewa zawadi ya kutwaa ubingwa wa michuano hiyo msimu uliopita ambapo ni dola 30,000 ambazo ni zaidi ya sh. Millioni 78 milioni.
“Sisi kama Singida BS tumethibitisha kushiriki mashindano hayo, tumeshawasiliana na viongozi wa CECAFA wamesema kuwa walipa zawadi yetu ya ubingwa kabla ya kuanza kwa mashindano hayo,” alisema Massanza.
Massanza alisema mashindano hayo, watayatumia kama sehemu ya maandalizi ya msimu ujao wa ligi kuu.
Singida Black Stars katika mashindano hayo ndio mabingwa watetezi baada ya msimu uliopita kuifunga Al Hilal ya Sudan kwa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa Dar es Salaam.
Mashindano ya mwaka huu yanatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na ushiriki wa baadhi ya mabingwa na vigogo wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku yakitumika kama kipimo muhimu kuelekea msimu mpya wa mashindano ya kimataifa ya CAF.




