Na NASRA KITANA
WAKATI Yanga ikimtambulisha Simo Dladla kuwa kocha msaidizi, klabu ya Simba imenasa saini ya mshambuliaji mzawa, Bakari Msimu kutoka klabu ya Coastal Union ya Tanga.
Taarifa zilizothibitishwa na klabu zote mbili, Dladla atafanya kazi chini ya Kocha Mkuu mpya wa timu hiyo, Manqoba Mngqithi kuhakikisha ubingwa wa Ligi Kuu Bara hauondoki mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.
Pia, Yanga imemtangaza kocha wa magolikipa, Greg Etafia kutoka Nigeria.
Yanga, imefanikiwa kumchukua Mtaalamu wa chambuzi wa Viwango na Mifumo ya Soka, Yardaan Valodia.
Hadi leo, Yanga imewasajili nyota wapya ambao ni Hussein Mihambo, Abdulnasir Mohamed wote kutoka Mashujaa FC ya Kigoma.
Yanga itakuwa na majukumu mengine ya kuhakikisha inafanya vizuri katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika(CAFCL) na Kombe la Shirikisho la CRDB lililoelekea Msimbazi msimu uliopita.
Lengo kuu la benchi hilo jipya la ufundi ni kuivusha Yanga kutoka hatua ya robo fainali waliyoizoea misimu ya hivi karibuni na kutinga hatua ya nusu fainali au fainali.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe alisema kuwa wana imani kubwa na kocha huyo kuwa atakuwa na msaada mkubwa katika kikosi chao.
Akizungumzia kuhusu kocha, Abdulhamid Moalin, Kamwe alisema bado ataendelea kusalia ndani ya kikosi hicho.
“Tumemtambulisha kocha mwenye CV kubwa kuwa msaidizi wa Mngqithi, hivyo tuna imani wataenda kushirikiana vyema ili kutimiza malengo tuliojiwekea msimu ujao,” alisema Kamwe.
Kwa upande wa Simba,Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally alisema kuwa wanaendelea kufanya usajili wa wachezaji wengi bora.
“Niwaambie tu mashabiki na wapenzi wa Simba kuwa tumesajili wachezaji wengi bora na wenye viwango hivyo wakae mkao wa kula kwani tutaendelea kushusha vifaa, kila siku,” alitamba.
Ahmed alisema Bakari Msimu amesaini mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kuongeza nguvu katika kikosi chao.
Tayari Simba imewasajili wachezaji wapya ambao ni Nathaniel Chilambo na Kelvin Nashon.
Wakati huo huo, Klabu ya Simba imemtangaza Emmanuel Nollo kama Mkurugenzi wa Wanachama na Mashabiki.




