Na MWANDISHI WETU
RAIS Dk. Samia Suluhu Hassan, ametoa wito kwa nchi za Afrika kuongeza uwekezaji wa ndani katika sekta ya afya, kujenga mifumo imara, endelevu na inayojitegemea kusimamia eneo hilo.
Dk. Samia alitoa wito huo, alipohutubia Mkutano Maalumu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kuhusu Afya, uliofanyika jijini Accra, nchini Ghana.
Mkutano huo, ulijadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa Ajenda ya Afya ya Afrika kupitia usawa katika upatikanaji huduma, afya kwa wote, kutokomeza ukimwi, kuboresha afya ya mama na mtoto na kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza na yasiyopewa kipaumbele.
Alisema Tanzania tayari imeanza kutekeleza Ramani ya Afya ya Umoja wa Afrika 2030 kwa kuiingiza katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/2027 – 2030/2031), huku ikijielekeza katika uwekezaji wa uzalishaji dawa, kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza uwezo wa nchi kujitegemea kwa huduma za afya.
“Afrika ina maarifa, rasilimali watu na uwezo wa kubadili mifumo yake ya afya. Tunachohitaji sasa ni utashi mkubwa wa kisiasa, uwekezaji wa ndani na mshikamano wa bara,” alisema.
Aidha, alisema serikali imefanya mageuzi ya sera na sheria kuvutia uwekezaji na kurahisisha biashara, hatua zilizowezesha kuanzishwa kwa viwanda 13 vya uzalishaji dawa huku wawekezaji 149 wakionesha nia ya kuwekeza nchini.
Pia, alisema Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imekuwa ya kwanza Afrika kufikia kiwango cha tatu cha ukomavu wa mifumo ya udhibiti wa 2/2 dawa wa Shirika la Afya Duniani (WHO Maturity Level 3), hatua inayotarajiwa kuharakisha uzalishaji wa dawa bora nchini na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya, Rais Samia alisema serikali imeongeza bajeti ya sekta hiyo kutoka sh. trilioni 1.8 mwaka 2024/2025 hadi sh. trilioni 3.1 mwaka 2026/2027, sambamba na kuanzisha bima ya afya kwa wote kuwawezesha wananchi, wakiwemo wenye kipato cha chini, kupata huduma muhimu za afya kwa gharama nafuu.
Alieleza kuwa, uwekezaji huo umewezesha kujengwa kwa hospitali za wilaya 119, vituo vya afya 649 na zahanati zaidi ya 2,700 na kuongeza idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya kutoka takriban 10,000 hadi 13,700 kufikia Machi mwaka huu.
Rais Samia, alisema uboreshaji huo, umechangia ongezeko la uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kutoka asilimia 65 hadi 86 na uzazi unaohudumiwa na wataalamu kutoka asilimia 66 hadi 85, huku vifo vya watoto chini ya miaka mitano vikipungua kutoka 147 hadi 43 kwa kila vizazi hai 1,000; na vifo vya kinamama vitokanavyo na uzazi vikipungua kutoka 556 hadi 104 kwa kila vizazi hai 100,000.
Akifungua mkutano huo, Rais wa Ghana, John Dramani Mahama, alisema kupungua kwa ufadhili wa afya duniani kunapaswa kuwa fursa kwa Afrika kuongeza uwekezaji wa ndani na kujenga mifumo ya afya inayojitegemea.
Rais Mahama aliahidi kumuunga mkono Rais Dk. Samia katika utekelezaji wa jukumu lake la Kinara wa Umoja wa Afrika wa Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, akisema uongozi wa Rais Dk. Samia utasaidia kuharakisha maendeleo katika eneo hilo.
Kadhalika, Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika na Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye, alizitaka nchi wanachama kuongeza uwekezaji katika huduma za afya za msingi na kuimarisha uwezo wa Afrika wa kuzuia, kugundua na kukabiliana na milipuko ya magonjwa.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Tedros Ghebreyesus, alisema maazimio ya mkutano huo yatakuwa na maana ikiwa yatafuatiwa na utekelezaji madhubuti, akisisitiza hatua zinazochukuliwa sasa zitakuwa msingi wa mustakabali wa afya barani Afrika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, alitoa wito kwa nchi wanachama kuharakisha ujenzi wa mnyororo wa uzalishaji bidhaa za afya barani humo ili kuongeza upatikanaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba na kuimarisha usalama wa afya wa bara hilo.




