Na Mwandishi Wetu, Misungwi
MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wilayani Misungwi, umesema miradi ya kunusuru kaya maskini iliyotekelezwa wilayani humo imeleta mabadiliko makubwa na nafuu ya kichumi kwa wananchi hususan wanufaika wake.
Hayo yameelezwa na Mratibu wa TASAF Wilaya ya Misungwi, Gloria Bunambi alipozungumza na waandishi wa habari na wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na mfuko huo, wakati wa wakiadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza umaskini duniani.
Gloria amesema miongoni mwa miradi hiyo imo ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, afya na barabara, pamoja na uwezeshaji wa kiuchumi unaolenga kupunguza umaskini katika jamii.
Akizungumza kuhusu mafanikio ya mpango huo, Gloria amesema mpango huo umesaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi, hususan katika maeneo ambayo awali yalikuwa na changamoto za miundombinu.
Amesema miongoni mwa mafanikio hayo ni ujenzi wa shule mpya ya sekondari ya wasichana yenye mabweni, madarasa, bwalo la chakula na maabara katika Kata ya Mabuki, hatua inayosaidia kupunguza umbali ambao wanafunzi walilazimika kutembea kufuata huduma za elimu.
Pia, amesema yamejengwa madarasa katika vijiji 10, huku miundombinu mingine ikihusisha ujenzi wa jengo la huduma za wagonjwa wa nje (OPD), nyumba ya mwalimu na uboreshaji wa barabara zilizokuwa na changamoto za kupitika.
Ameeleza kuwa uboreshaji barabara umesaidia kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo kutoka vijijini kwenda katika masoko, hivyo kuchangia shughuli za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Mbali na miradi ya miundombinu, amesema TASAF imekuwa chachu ya kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato kupitia vikundi vya kiuchumi vinavyojishughulisha na shughuli mbalimbali za uzalishaji.
Aidha, amesema kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), wananchi wamepatiwa mafunzo ya ujasiriamali na utengenezaji wa bidhaa kama sabuni za kufulia na kuogea, mafuta ya kujipaka, batiki na viungo vya chakula, hatua inayowawezesha kuanzisha biashara na kupanua shughuli za uzalishaji.
Kwa mujibu wa Gloria, baadhi ya vijiji vilivyonufaika na mafunzo hayo ni Mapilinda, Kali na Igenge, ambako wananchi wamepata ujuzi wa kutengeneza bidhaa kwa matumizi na biashara.
Ofisa huyo amefafanua kiwa, wananchi wengine wamejikita katika ufugaji wa mbuzi na kondoo, kilimo cha bustani, mpunga na mazao mengine, huku wengine wakifanya biashara ndogondogo.
“Shughuli hizo zimewasaidia baadhi ya walengwa kuongeza kipato na kuwekeza katika shughuli zinazoweza kuendeleza uchumi wa kaya zao,” alieleza.
Ameongeza kuwa, mafanikio ya mpango huo yanaonekana pia katika uwezeshaji wa vikundi kupata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri kuendeleza shughuli za kiuchumi.
“Hadi mwaka 2026, vikundi 10 vilikuwa vimenufaika na mikopo hiyo katika Wilaya ya Misungwi, huku vikundi vingine vikiendelea na taratibu za kuomba mikopo,” amebainisha.




