NA LILIAN JOEL, Arusha
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetoa wito kwa viongozi wake kuzingatia maadili, nidhamu na mwenendo unaolinda heshima ya Chama.
Katibu wa NEC Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, alisema hayo, alipofungua mafunzo kwa viongozi na wanachama wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini.
Amesema viongozi wanapaswa kuzingatia katiba, kanuni na misingi ya Chama katika utekelezaji wa majukumu yao na maisha ya kila siku.
“Viongozi wa CCM kuanzia ngazi za mikoa, wilaya, kata, jumuiya na mabalozi, mnatakiwa kutambua nafasi za uongozi zinahitaji nidhamu, kujitambua na kuwa mfano bora kwa jamii inayowazunguka,”amesema.
Amesema viongozi wanaposhindwa kujidhibiti na kujihusisha na tabia zisizofaa, hasa maeneo ya starehe, wanaweza kukidhalilisha Chama.
“Ukishakuwa kiongozi, lazima uwe na kiasi katika kila jambo, haiwezekani unakwenda kwenye maeneo ya starehe unatumia vilevi kupita kiasi.
“Wakati mwingine eneo hilo linapotakiwa kufungwa unajigamba huoni CCM iko hapa. Hii haikubaliki, lazima kila mmoja wetu azingatie maadili na Katiba ya Chama chetu,”ameongeza.
Kuhusu mafunzo hayo, Kihongosi alisema ni sehemu muhimu ya kuimarisha uelewa wa viongozi, wanachama kuhusu itikadi, historia ya CCM na misingi yake hasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2030.
AMANI
Kihongosi aliwataka vijana kutumia busara na kutafakari kwa kina, kabla ya kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.
“Vijana lindeni amani ya nchi, wapo umri wa miaka 20, 30 na 40 bado wana miaka mingi ya kuishi, kufanya kazi na kulea familia zao.
“Hivyo mnapaswa kuzingatia mustakabali wetu na vizazi vijavyo kabla ya kufanya maamuzi yanayoweza kuvuruga utulivu wa nchi,” alisema.
MITANDAO
Vilevile, Kihongosi aliwataka viongozi na wanachama wa CCM, kutumia mitandao ya kijamii kwa kuelimisha wananchi kuhusu sera, mipango, utekelezaji wa shughuli za serikali kwa kutoa taarifa sahihi zinazothibitishwa kwa takwimu na ushahidi.
“Baadhi ya watu wanatumia mitandao ya kijamii kupotosha umma na dunia juu ya kazi kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na CCM.
“Rai yangu kwenu wana CCM, tunawajibu kwa hoja na ushahidi badala ya kuingia katika malumbano yasiyo na tija,”alisema.
USAJILI
Kuhusu usajili wa wanachama tangu mafunzo hayo yalipoanza Oktoba 9 hadi Oktoba 16, mwaka huu katika wilaya mbalimbali nchini, alisema wamesajili zaidi ya wanachama wapya 78,000.
MIRADI
Katika hatua nyingine, Kihongosi aliwataka viongozi kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2025-30 katika maeneo yao.
“Mkoa wa Arusha, serikali imeleta fedha nyingi za kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo, zikiwemo barabara za njia nne. “Ni wajibu wenu kufuatilia kuwa thamani ya fedha inaonekana kwa maslahi mapana ya wananchi,” aliongeza.
KATIBU WA CCM ARUSHA
Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha Mjini, Timoth Sanga, alisema wamesajili wanachama 764 sawa na asilimia 158.2.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arumeru, Noel Severe, amesema wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Diwani wa Kata ya Olorieni, Hendry Sikoi.
Sikoi alifariki dunia juzi Jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipapatiwa matibabu.
Alichaguliwa mara ya kwanza kuwa diwani wa kata hiyo mwaka 2025.




