Na MUSSA YUSUPH,
Songwe
KATIBU Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo, amesema CCM kimemchangua Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kugombea Urais kwa sababu ni kiongozi mwenye nguvu ya kuivusha nchi salama.
Chongolo ambaye pia ni mgombea Ubunge katika Jimbo la Makambako mkoani Njombe, amesema Rais Dk. Samia ametekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM (2020 – 2025) kwa mafanikio makubwa.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Tunduma mkoani Songwe, Chongolo amesema Watanzania wapo tayari kumpigia kura za kishindo katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
“Chama kimemsimamisha Rais Samia kupeperusha bendera kwenye uchaguzi mkuu kwasababu ana nguvu ya kuivusha nchi salama. Nguvu uliyonayo ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 ambayo umeitekeleza vizuri na kwa weledi. Kwa uliyoyafanya huna haja ya kupiga kampeni, nenda kapumzike mambo ya ukanda huu (nyanda za juu kusini) utayaona katika matokeo baada ya Oktoba 29 mwaka huu,” amesisitiza.
“Mwaka 2020/21, hakukuwa na ruzuku ya pembejeo lakini kutokana na uamuzi mkubwa wa Rais Samia kuwajali wakulima ili wasibebe mzigo, imefanya wananchi kuwa na kazi ya kulima ambapo sasa kuna ziada ya chakula,” amebainisha.
Kuhusu sekta ya afya, amesema wananchi wa Songwe wameendelea kupata huduma za afya baada ya imarishaji wa sekta hiyo kwa kila hospitali ya wilaya kujengwa jengo la huduma za dharura.
Pia, Chongolo ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe, amesema Rais Dk. Samia amewezesha watoto wa Kitanzania kupata elimu bila kikwazo baada ya kuwezesha upatikanaji elimu hadi kidato cha sita bila ada.
Vilevile, amesema Dk. Samia ameifungua Songwe kwa kujenga barabara ya Isongole – Ileje inayojengwa kwa gharama ya sh. bilioni 79 na ile ya kuunganisha Mkoa wa Mbeya kupitia Wilaya ya Kyela ambako kazi inaendelea.
Kadhalika, amesema serikali inajenga barabara ya Mlowo – Kamsamba ambayo ilishapata mkandarasi pamoja na barabara ya Mbeya – Songwe kupitia Mbalizi.
Katibu mkuu huyo mstaafu amesema Rais Dk. Samia ameimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato ambapo kituo cha forodha cha Tunduma kimeongeza ukusanyaji mapato kutoka sh. bilioni 139 hadi kufikia sh. bilioni 204 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.




