NA MUSSA YUSUPH,
Bahi
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan, amesema serikali imeimarisha zaidi miundombinu ya barabara katika kipindi cha miaka mitano.
Dk. Samia aliyasema hayo katika mkutano wake wa kampeni uliofanyika wilayani Bahi mkoani Dodoma alipokuwa njiani kwenda mkoani Singida.
Alisema katika wilaya hiyo, yamejengwa madaraja tisa na barabara za changarawe zenye urefu wa kilometa 152 zinazopitika kipindi chote cha mwaka.
“Nimejulishwa kuna barabara ya Mwanachungu- Bahi hadi SGR yenye urefu wa kilometa sita ambako kuna changamoto kuvuka eneo la Mto Mkogwa wakati wa masika.
“Hii barabara tumeipanga kuijenga kwa awamu mbili, tutaanza kujenga daraja la Mto Mkogwa ambalo limekuwa kero kubwa katika maeneo hayo,” alisema.
Dk. Samia alisema usanifu wa daraja hilo, umekamilika kazi iliyopo ni kuanza ujenzi kisha litakapokamilika barabara hiyo itajengwa.
Akizungumzia miundombinu, mgombea ubunge Jimbo la Bahi, Kenneth Nollo, alisema barabara nyingi zimeboreshwa na madaraja kujengwa, hatua iliyorahisisha usafiri na shughuli za kiuchumi.
Hata hivyo, aliomba serikali kuongeza ujenzi wa barabara za lami katika mji wa Bahi kuupa hadhi zaidi.
“Ombi langu kwa serikali ni kutupatia angalau kilomita tano za barabara ya lami, kuuboresha mji wetu wa Bahi ambao unaendelea kukua kwa kasi,” alisema.
Katika sekta ya elimu, alisema shule mpya 14 zimejengwa wilayani humo, jambo linaloonesha jitihada kubwa za serikali katika kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Bahi.
Nollo alieleza kufurahishwa na ujenzi wa kituo cha SGR na bandari kavu katika eneo hilo, akisema uwekezaji huo unaifanya Bahi kuwa kitovu muhimu cha biashara na uchukuzi.




